Hamburg yajitoa kutoka mkiani Bundesliga
4 Mei 2015Ligi ya Ujerumani imebakiza sasa michezo mitatu kufika mwisho na suala si nani bingwa , lakini ni timu gani itabakia katika ligi hiyo baada ya timu zipatazo 5 kuwamo katika hatari ya kushuka daraja na kwa hiyo shauku imehamia mkiani mwa ligi hiyo, wakati , VFL Stuttgart, Hannover 96 , FC Freiburg , SC Pardaborn na Hamburg SV kila moja inaweza kutumbukia katika ligi daraja la pili katika michezo mitatu iliyobaki.
Lakini jana Jumapili SV Hamburg ilijitutumua na kufanikiwa kupata ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Mainz 05 na kujitoa kutoka katika nafasi ya tatu kutoka mwisho na kupanda hadi nafasi ya 14. Kocha Bruno Labbadia alikuwa na haya ya kusema kuhusu ushindi huo muhimu.
"Naamini ni nia thabiti. Tulihitaji kwa udi na uvumba ushindi. Tulijaribu kwa mara nyingine tena kila kitu, na pia tulikuwa kidogo tumechoka. Lakini naweza kusema , timu ilihitaji ushindi kwa hali yoyote ile.
SC Pardaborn ikiwa timu yenye bajeti ndogo kabisa katika Bundesliga nayo pia inapiga hatua kuelekea kubakia katika ligi hiyo baada ya kupanda kutoka nafasi ya pili kutoka mwisho hadi nafasi ya 15 nyuma ya Hamburg. Hannover licha ya kutoka sare na Wolfsburg iliyoko nafasi ya pili baada ya mabingwa Bayern Munich imeteremka hadi nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na maana imetumbukia katika hatari kamili ya kushuka daraja.
Kocha mpya wa Hannover 96 Michael Frontzeck anasema hajakata tamaa kubakia daraja la kwanza.
"Kama nimefuatilia vizuri, Wolfsburg ilikuwa na nafasi moja ama zaidi ya kufanya matokeo kuwa 3-2. Lakini pande zote mbili zingeweza kushinda. Natoa sifa nyingi kwa timu yangu, kwa kuweza kurejesha mabao na kurejea katika mchezo. Ni vigumu kufanya hivyo hapa, nadhani kila timu imeshindwa ilipocheza hapa. Wakiwa nyumbani timu yao ni imara sana. Na hii inanifanya nijisikie vizuri. Wiki iliyopita tulishindwa kwa bahati mbaya kabisa na muhimu ni kwamba tumepata pointi, tayari kwa mchezo muhimu dhidi ya Bremen."
Kulikuwa pia na mpambano wiki hii wa kuwania nafasi za kucheza katika ligi ya Ulaya, Europa League, ambapo makamu bingwa wa msimu uliopita Borussia Dortmund baada ya kuifungashia virago Bayern Munich katika kombe la shirikisho DFB Pokal katikati ya wiki iliyopita, ilikuwa na kibarua cha kuiondoa TSG Hoffenheim kutoka nafasi hiyo. Lakini vijana wa TSG Hoffenheim walikataa katu katu na mchezo huo uliamuliwa kwa sare ya bao 1-1.
Kevin Volland ni mshambuliaji wa Hoffenheim.
"Nafasi zilikuwapo. Hususan katika kipindi cha pili tuliweza kuweka mbinyo wa kutosha. Pia katika kipindi cha kwanza tulicheza vizuri, hatukuwapa Dortmund nafasi. Kwa hiyo ni bahati mbaya, kwamba hatukuweza kutoka na pointi tatu. Kwa upande mwingine pointi tuliyopata inatufanya tujisikie vizuri , na sasa tutapaswa kuendelea kufanya hivyo dhidi ya Frankfurt."
Borussia Moenchengladbach ilirejea katika nafasi ya tatu juu ya msimamo wa ligi jana Jumapili baada ya kuishinda Hertha Berlin kwa mabao 2-1 na kuiondoa Bayer Leverkusen katika nafasi hiyo , licha ya ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa tena wa ligi ya Bundesliga Bayern Munich siku ya Jumamosi.
Uamuzi hata hivyo utapatikana wiki ijayo ambapo Borussia Moenchengladbach itakuwa mwenyeji wa Bayer Leverkusen kuamua ni timu ipi itachukua nafasi hiyo ya tatu.
Wakati huo huo mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Max Kruse atajiunga na VFL Wolfsburg kutoka Borussia Moenchengladbach msimu ujao baada ya kuthibitishwa kwamba amefanya uchunguzi wa afya na klabu yake hiyo mpya .
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae /
Mhariri: Daniel Gakuba