Hamas yafufua uhusiano na utawala wa Syria
11 Oktoba 2022Hatua ya Hamas inajiri huku kukiwa na mabadiliko ya kimsingi katika uhusiano wa Mashariki ya Kati ambayo yalishuhudia mshirika wa muda mrefu wa kundi hilo Uturuki, ikirejesha uhusiano kamili wa kidiplomasia mwezi Agosti na Israel, adui mkuu wa kundi la wanamgambo hao wa wanaotawala katika ukanda wa Gaza.
Ujumbe unaoongozwa na maafisa wa Hamas unatarajiwa katika mji mkuu wa Syria wiki ijayo, kufuatia mfululizo wa mikutano ya maandalizi.
Hamas inajiona kuwa inaongoza upinzani wa silaha dhidi ya Israel na mzingiro wake dhidi ya Gaza, lakini inachukuliwa kuwa kundi la kigaidi na Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya.
Soma pia: Hamas yasema bado mapambano yanaendelea Gaza
Kundi hilo mwezi uliopita lilisifu uhusiano wake mpya na utawala wa Syria wa Bashar al-Assad kama "huduma kwa taifa (la Palestina) ambalo watu wake pia wanaishi chini ya ukaliaji wa Israel katika Ukingo wa Magharibi.
Hamas ilitaja "maendeleo ya haraka ya kikanda na kimataifa kuhusu mapambano yetu na taifa letu" -- bila kutaja moja kwa moja uhusiano uliorejeshwa kati ya Israel na Uturuki na uhusiano na mataifa kadhaa ya Kiarabu.
Mabadiliko hayo yanakuja wakati mshirika wa Syria Iran, ambayo sasa imekumbwa na wimbi la maandamano, inakinzana vikali na mataifa ya Magharibi na baadhi ya mataifa yenye nguvu katika kanda hiyo, hasa kuhusu mpango wake wa nyuklia, ambao Israel inauona kuwa tishio kwa uwepo wake.
Uongozi wa Hamas, ambayo imetawala eneo lililokumbwa na umaskini la Gaza tangu mwaka 2007, umekuwa ukiishi nje ya nchi kwa muda mrefu huku jeshi la Israel likishambulia mara kwa mara maeneo ya wanamgambo katika eneo hilo.
Soma pia: Israel, Wanamgambo wa Palestina wakubali kusitisha mapigano
Hamas ilikuwa na makao yake makuu mjini Damascus lakini iliyafunga mwaka 2012 baada ya kundi hilo lililotoka katika vuguvugu la Udugu wa Kiislamu kuegemea upande wa upinzani dhidi ya Assad.
Viongozi wake kisha walihamia katika taifa la Ghuba la Qatar na Uturuki, ambayo yalikuwa yamekata uhusiano na Israel kutokana na uvamizi wa kikatili wa makomando wa Israel dhidi ya meli ya msaada ya Uturuki iliyojaribu kuvunja kizuizi cha bahari ya Gaza.
Ujumbe wa Hamas unaotarajiwa mjini Damascus wiki ijayo utaongozwa na Khalil al-Hayya, mkuu wake wa uhusiano wa Kiarabu, alisema Khaled Abdel Majid, mkuu wa kundi la Palestinian Popular Struggle Front, ambalo liko karibu na utawala wa Syria.
Uamuzi wa Hamas kushirikiana tena na Damascus unafuatia ziara nyingi za maafisa wake nchini Syria, "za siri na hadharani", chanzo cha Hamas kiliiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina.
Iran inaimarisha mhimili wake wa upinzani
Mikutano hiyo ilipatanishwa na Iran na Hezbollah, ambao wote wamepigana upande wa Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, chanzo hicho kilisema.
Soma pia: Pande pinzani nchini Palestina zaandaa mkutano wa pamoja kuhusu Israeli na UAE
Haya yote yanaakisi nia ya Iran ya kuimarisha "mhimili wa upinzani" ambao pia unajumuisha kundi la Wapalestina la Islamic Jihad, alisema Mukhaimer Abu Saada, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar cha Gaza.
Huku mazungumzo ya Iran ya kurejesha mapatano yake ya nyuklia yaliyovurugika mwaka 2015 na mataifa makubwa yakidorora, imegeuka karibu na Urusi, ambayo pia inakabiliwa na kuzidi kutengwa kimataifa kutokana na vita vyake nchini Ukraine.
Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh, mwenye makao yake nchini Qatar, mwezi uliyopita alisafiri kwenda Moscow na alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.
Wakati kundi hilo likirejea Syria, chanzo kikuu cha Hamas kiliiambia AFP, inapanga "kufungua ofisi ya mwakilishi mjini Damascus hivi karibuni, kama hatua ya kwanza ya kurejea kwa uhusiano wa kawaida".
Soma pia: Hamas yafyatua zaidi ya maroketi 200 kuelekea Israel
Mkuu wa zamani wa kisiasa wa Hamas, Khaled Mashal, aliwahi kufurahia upendeleo wa nadra mjini Damascus na alikuwa na uhusiano wa kibinafsi na Assad.
Hata hivyo, bado kuna uwezekano mdogo kwamba utawala wa Syria utairuhusu Hamas kujijenga tena na kuwa uzito iliyokuwa nayo muongo mmoja uliyopita", alisema Jamal al-Fadi, pia profesa wa siasa katika chuo kikuu cha Al-Azhar.
Uongozi wa Hamas pia unaweza kuhofia kutumia muda mwingi nchini Syria, ikizingatiwa kwamba Israel hufanya mashambulizi nchini mara kwa mara, hasa ikiwalenga wapiganaji wanaoiunga mkono Iran.
"Uhusiano wa Hamas na Syria kwa sasa utakuwa chini ya mazingatio magumu ya kiusalama," alisema Fadi. "Inawaweka hatarini viongozi na wanaharakati wake kulengwa kwa urahisi na Israel."
Soma pia:Vizuizi vya Israel ukanda wa Gaza vimeathiri uchumi
Uhusiano unaochipukia tena kati ya Hamas na Syria umefichua mpasuko ndani ya vuguvugu hilo la Kiislamu. Saleh al-Naami, profesa wa siasa katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza ambaye yuko karibu na Hamas, aliuelezea mpango huo na Damascus kama "dhambi ya kimaadili".
"Pia hauakisi msingi wa vuguvugu hilo na idadi kubwa zaidi ya wasomi wake (wa kisiasa)," aliandika kwenye Twitter.
Hata hivyo, mkuu wa kamati ya kisiasa ya Hamas, Bassem Naim, alisema uamuzi huo ulifuatia miaka mingi ya mijadala ya kikanda na kimataifa.
"Mwishowe, Hamas ilikwenda na maoni ya wengi juu ya kuanzishwa tena kwa uhusiano na Syria," alisema Naim. "Hakuna chaguo, bali kwa Hamas kuwa katikati ya mhimili wa upinzani."
Chanzo: AFPE.