Hamas yaahidi kuendelea na mazungumzo hadi makubaliano
6 Machi 2024Wawakilishi wa Hamas na Marekani wamekuwa wakikutana na wapatanishi wa Qatar na Misri mjini Cairo kujadiliana mpango wa kusitisha mapigano kwa kipindi cha wiki sita, mabadilishano ya mateka waliosalia mikononi mwa Hamas kwa mamia ya wafungwa wa Kipalestina walio mikononi mwa Israel na upelekaji mkubwa zaidi wa misaada kwenye Ukanda wa Gaza.
Kituo cha televisheni cha Al-Qahera News, ambacho kina mafungamano na shirika la ujasusi la Misri, kilisema mazungumzo hayo yalikuwa yaendelee siku ya Jumatano (Machi 6).
Kwa upande wao, viongozi wa Hamas walisema wangeliendelea na majadiliano hadi pale makubaliano ya kusitisha mapigano yatakapofikiwa.
"Vuguvugu letu litaendelea na mazungumzo kupitia ndugu zetu wapatanishi ili kufikia makubaliano yanayokidhi matakwa na masharti ya watu wetu", lilisema kundi hilo kwenye taarifa yake ya Jumatano.
Hata hivyo, kwenye taarifa hiyo waliilaumu Israel, ambayo haikutuma wawakilishi wake mjini Cairo, kwa kukwepa kile walichosema ni "hoja kuu kwenye mazungumzo haya."
Hamas imekuwa ikisisitiza kuwepo kwa usitishaji wa kudumu wa mapigano, kurejea nyumbani kwa wakimbizi wa Kipalestina, kujiondowa kwa Israel kwenye Ukanda wa Gaza na kuwapatia Wapalestina mahitaji yote muhimu.
Marekani yaishinikiza Hamas kukubali usitishaji mapigano
Kauli ya Hamas ilitolewa ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye taifa lake ndilo muungaji mkono na mfadhili mkubwa wa Israel, kulitaka kundi hilo likubali haraka kufikia muafaka na Israel.
"Hili suala sasa liko mikononi mwa Hamas. Kunapaswa kuwepo kwa usitishaji mapigano kwa sababu kama hali hii ikiendelea hadi Ramadhani, Israel na Jerusalem zinaweza kuwa kwenye hatari kubwa sana kabisa." Alisema rais huyo wa Marekani akiwa mjini Maryland siku ya Jumanne (Machi 5).
Biden alikuwa akiakisi kauli kama hiyo iliyotolewa na waziri wake wa mambo ya nje, Antony Blinken, ambaye naye alikuwa ameisihi Hamas kukubaliana na kile alichokiita "usitishaji wa haraka wa mapigano."
Uwezekano wa machafuko ya Al-Aqsa
Ingawa Biden hakufafanuwa zaidi kauli yake, lakini wiki iliyopita, Marekani iliitaka Israel kuwaruhusu Waislamu kuswali kwenye Msikiti wa Al-Aqsa ulioko Jerusalem, eneo ambalo limekuwa kituo cha machafuko katika mwezi wa Ramadhani.
Serikali ya Israel ilisema siku ya Jumanne kwamba ingeliwaruhusu waumini wa Kiislamu kuingia kwenye eneo la msikiti huo kwa idadi ile ile ya wanaoswali swala nyengine, hii ikimaanisha kuwa isingeliruhusu idadi kubwa zaidi ya hiyo.
Kudhibiti idadi ya wanaoswali kwenye msikiti huo ni kinyume na matakwa ya waumini wenyewe wa Kiislamu wanaouchukulia mwezi wa Ramadhani kuwa kipindi maalum cha ibada, ambacho hujazana misikitini.
Kwenyewe Gaza, wizara ya afya ilisema siku ya Jumatano kwamba watu waliokwishauawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel katika Ukanda huo wamefikia 30,717.
Hiyo ni baada ya wengine 86 kuuawa ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
Jumla ya watu 72,156 wameripotiwa kujeruhiwa ndani ya kipindi cha miezi mitano ya mashambulizi hayo.
AFP, dpa