1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas na PLO wakubaliana kuunda umoja wa kitaifa

Abdu Said Mtullya23 Aprili 2014

Wapalestina za Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza wamefikia makubaliano ya kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa katika muda wa wiki tano zijazo wakati ambapo mazungumzo na Israel yamo katika hatari ya kuvunjika.

https://p.dw.com/p/1BnUn
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na kiongozi wa Hamas Ismail Haniya
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na kiongozi wa Hamas Ismail HaniyaPicha: picture-alliance/dpa

Hii si mara ya kwanza kwa pande hizo hasimu kutangaza makubaliano juu ya kuimaliza miaka saba ya kutengana kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa magharibi.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika mji wa Gaza hadi alfajiri ya jumatano baina ya viongozi wa Hamas na wa chama cha ukombozi wa Palesttina PLO.

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniya amesema kwa makubaliano hayo Wapalestina wameumaliza mgawanyiko. Amesema mkataba huo umefikiwa haraka kwa sababu Wapalestina wametaka iwe hivyo.

Bwana Haniya ameleza kuwa makubaliano yaliyofikiwa ni ishara kwamba Wapalestina wamezimudu changamoto na matatizo yao.Pia ni msingi wa ushirikiano sahihi baina ya pande zote za kisiasa za Wapalestina"

Netanyahu akasirika

Hatua ya viongozi wa Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi kufikia mapatano na Hamas imemkasirisha Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Waziri Mkuu Netanyahu amesema Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wanaonyesha kuwa hawana dhamira ya kuyanusru katika dakika za mwisho mazungumzo ya kuleta amani katika Mashariki ya Kati yanayofanyika kwa upatanishai wa Marekani.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/dpa

Netanyahu amemlaumu Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas kwa alichosema kufikia mapatano na Hamas badala ya kufikia mapatano na Israel. Netanyahu amesema Rais Abbas anapaswa kuchagua.Jee anataka amani na Hamas ama na Israel? Netanyahu amemwambia Abbas kwamba anaweza kuchagua moja tu.

Lakini mwakilishi mkuu wa Palestina kwenye mazungumzo na Israel Saeb Erakat amejibu kwa kusema kwamba haitawezekana kuleta amani na Israel bila ya umoja wa Wapalestina.

Uchaguzi wa Rais na Bunge

Hata hivyo viongozi wa Hamas na wa PLO walikutana tena leo kujadili uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa Rais na wa Bunge katika maeneo yote ya Wapalestina. Pia walijadili suala la kuiingiza Hamas katika PLO.

Pande hizo hasimu za Hamas na PLO zilitangaza mara kwa mara hapo awali juu ya kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya umoja ya wataalamu, lakini aghalabu lengo hilo lilishindikana. Safari hii pia wachunguzi wana mashaka iwapo mambo yatakuwa tafauti na hapo awali.

Mwandishi: Mtullya Abdu/afpe

Mhariri: Yusuf Saumu