1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas haitashiriki mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza

14 Agosti 2024

Kundi la Hamas limesema halitoshiriki katika duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yaliyopangwa kufanyika Alhamisi huko Qatar, na kuondoa matumaini ya kupatikana kwa makubaliano hayo.

https://p.dw.com/p/4jSud
Kiongozi wa Hamas, Yahya Sinwar
Kiongozi wa Hamas, Yahya SinwarPicha: Ahmed Zakot/SOPA Images via ZUMA Press/picture alliance

Marekani imesema inatarajia mazungumzo hayo yasiyo ya ana kwa ana yataendelea kama yalivyopangwa kwenye mji mkuu wa Qatar, Doha, na kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano bado yanawezekana. Hata hivyo, tovuti ya habari ya nchini Marekani, Axios imeripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, ameahirisha ziara yake Mashariki ya Kati ambayo ilikuwa ianze Jumanne.

Maafisa watatu wa ngazi ya juu wa Iran wamesema makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza ndiyo jambo pekee litakaloifanya Iran isilipize kisasi dhidi ya Israel, ambayo inaishutumu kwa mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh mjini Tehran, mwezi uliopita.

Israel kupeleka ujumbe kwenye mazungumzo

Serikali ya Israel imesema itapeleka ujumbe wake kwenye mazungumzo ya Alhamisi, lakini Hamas, kundi linaloidhibiti Gaza, linataka kuwepo kwa mpango wa kutekeleza pendekezo ambalo tayari imelikubali, kuliko kushiriki kwenye mazungumzo zaidi.

Afisa wa ngazi ya juu wa Hamas, Sami Abu Zuhri ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Hamas imejizatiti katika pendekezo lililowasilishwa kwake Julai 2, ambalo linatokana na azimio la Baraza la Usalama la Marekani na hotuba ya Rais Joe Biden, na kwamba kundi hilo limejiandaa kuanza mara moja mazungumzo kuhusu utaratibu wa kulitekeleza. Abu Zuhri amesema kushiriki mazungumzo mapya kutaruhusu kuwekwa masharti mapya na kutumia mazungumzo kadhaa kuendelea kufanya mauaji zaidi.

Mjumbe maalum wa Marekani Amos Hochstein, akiwa na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri
Mjumbe maalum wa Marekani Amos Hochstein, akiwa na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih BerriPicha: Bilal Hussein/AP Photo/picture alliance

Kwa upande wake mjumbe maalum wa Marekani Amos Hochstein amesema anaamini kuwa vita kati ya Israel na kundi la Hezbollah la Lebanon, vinaweza kuepukika, lakini Israel na Hamas zinahitaji kuelekea kwenye makubaliano ya amani ya Gaza bila kuchelewa zaidi. Hochstein yuko mjini Beirut kwa lengo la kupunguza mvutano kati ya Israel na Hezbollah, baada ya mauaji ya kamanda wa kijeshi wa Hezbollah Fuad Shukr mjini Beirut, mwezi uliopita.

''Tunaendelea kuamini kuwa azimio la kidiplomasia linaweza kufikiwa kwa sababu tunaendelea kuamini kwamba hakuna mtu anayetaka kweli vita kamili kati ya Lebanon na Israel,'' alisisitiza Hochstein.

Hochstein akutana na Spika wa Bunge la Lebanon

Hochstein ameyazungumza hayo, baada ya kukutana na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, mshirika muhimu wa Hezbollah. Amesema pande zote zinapaswa kuwa na uwezo wa kufanya hivyo, kwa usalama, na wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa hatua za kidiplomasia na ufumbuzi wa kidiplomasia, na kwamba wakati huo ni sasa.

Aidha, katika uwanja wa mapambano, maafisa wa afya wa Palestina wamesema mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza, yamewaua takribani watu 17, wakiwemo watoto watano na wazazi wao. Mashambulizi hayo yametokea kwenye kambi za wakimbizi za Nuseirat na Maghazi, huku mashambulizi mengine yakiripotiwa Khan Yunis na Beit Lahiya.

(AFP, DPA, AP Reuters)