Hali yazidi kutisha Myanmar
28 Machi 2021Waandamanaji nchini Myanmar wamerudi tena kwenye maandamano mitaani wakishinikiza madai yao ya kutaka demokrasia irudishwe,ikiwa ni siku moja baada ya vikosi vya usalama kusababisha umwagaji mkubwa wa damu kwa kuwauwa zaidi ya watu 100.
Umwagikaji huo wa damu ndio mkubwa zaidi kutokea tangu mapinduzi ya jeshi nchini humo mwezi Uliopita. Maandamano siku ya Jumapili yameshuhudiwa Yangon na Mandalay miji miwili mikubwa kabisa nchini humo na maeneo mengine. Baadhi ya waandamanaji walipambana tena na vikosi vya polisi.
Inaarifiwa kwamba takriban watu 114 waliuwawa Jumamosi wakati jeshi la polisi lilipowaandama waandamanaji waliokuwa wamejitokeza kupinga mapinduzi ya Februari Mosi yaliyomuondowa madarakani Aung San Suu Kyi na serikali yake iliyochaguliwa na wananchi. Miongoni mwa waliouwawa ni pamoja na watoto wengi waliokuwa chini ya umri wa miaka 16 kwa mujibu kituo cha habari cha mtandaoni cha Myanmar.
Takwimu sawa na hiyo ya waliouwawa imetolewa pia na vyomvo vingine vya habari vya Myanmar ba watafiti ikiwa ni idadi kubwa ya watu waliouwawa ikilinganishwa na mauaji yaliyofanyika March 14. Kwa ujumla imeelezwa kwamba waliouwawa nchini humo tangu mapinduzi ya kijeshi ni watu 420 kwa mujibu wa vyanzo mbali mbali. Mapinduzi ya Myanmar yamebadilisha kabisa hatua zilizopigwa miaka kadhaa kuelekea demokrasia baada ya miongo mitano ya nchi hiyo kuwa chini ya utawala wa kijeshi na kuifanya tena nchi hiyo kumulikwa na Jumuiya ya kimataifa.
Mauaji ya jumamosi yaliyofanywa na jeshi la polisi na wanajeshi yameshuhudiwa nchi nzima wakati jeshi la nchi hiyo likiwa linaadhimisha sikukuu ya kila mwaka ya siku ya jeshi kwa kufanyika gwaride maalum katika mji mkuu wa nchi hiyo Naypyitaw. Umwagikaji huo wa damu umelaaniwa na jumuiya ya kimataifa kupitia ofisi za kidiplomasia ndani ya Myanmar na nje ya nchi hiyo.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ameshtushwa na mauaji hayo ya raia ikiwemo watoto na kusisitiza kwamba ukandamizaji unaofanywa na jeshi haukubaliki na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua msimamo thabiti wa pamoja kuchukua hatua.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken kupitia ujumbe wa Twitta amesema nchi yake imetamaushwa na umwagikaji damu uliofanywa na vikosi vya Usalama ambavyo vimeonesha utawala huo wa kijeshi utayatoa rehani maisha ya raia wasio na hatia kuwatumikia wachache.
Lakini pia wakuu wa majeshi kutoka nchi nyingine 12 wametoa taarifa ya pamoja kulaani matumizi ya nguvu dhidi ya raia. Mawaziri wa ulinzi wa Australia,Canada,Ujerumani,Ugiriki,Italia,Japan,Denmark,Uholanzi, Newzealand,Korea Kusini,Uingereza na Marekani wametoa taarifa wakitowa mwito wa pamoja wa kulitaka jeshi la Myanmar kuacha kabisa matumizi ya nguvu na kuchukua hatua ya kurudisha heshima na imani ya wananchi waliyoipoteza kutokana na vitendo vyao.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Amnesty International limeikosoa tena jumuiya ya kimataifa likisema haichukui hatua za kutosha kumaliza vurugu nchini Myanmar. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani machafuko ya Myanmar lakini halijazungumzia juu ya kutaka hatua thabiti zichukuliwe dhidi ya utawala wa kijeshi nchini humo,mfano kuzuia nchi hiyo kuuziwa silaha.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Sudi Mnette