1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya Ebola inazidi kuwa mbaya zaidi

28 Agosti 2014

Mataifa matatu ya Afrika Magharibi yanayokabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola yameendelea kujikuta katika hali ya kutengwa wakati mashirika zaidi ya ndege yakisitisha safari zake katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/1D2ya
Liberia Ebola 24.08.2014
Picha: John Moore/Getty Images

Hayo yanajiri wakati Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa nchini Marekani akionya kuwa hali itakuwa mbaya hata zaidi kama hatua za dharura hazitochukuliwa katika kupambana na mlipuko wa virusi vya ugonjwa huo hatari.

Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa nchini Marekani Tom Frieden ameonya kuwa janga la ugonjwa wa Ebola nchini Liberia litaendelea kuwa mbaya hata zaidi kwa sababu visa vingi havijatambuliwa na kuripotiwa kwa maafisa wa afya. "ipo haja ya kuchukua hatua ya dharura. Ulimwengu haujawahi kuona mripuko wa Ebola kama huu. Natamani nisingesema hili, lakini hali itaendelea kuwa mbaya, kabla ya utulivu kurejea".

Wakati huo huo, Shirika la ndege la Ufaransa - Air FRANCE limelikubali ombi la serikali ya Ufaransa la kulitaka “lisitishe kwa muda” huduma zake nchini Sierra Leone, na kuuwacha mji mkuu wa nchi hiyo Freetown na Monrovia katika nchi jirani Liberia na safari moja tu ya kawaida kutoka kwa Shirika la ndege la Royal Air Morocco.

Ebola Universitätsklinikum Hamburg Eppendorf WHO
Mgonjwa wa Ebola akiwasili katika hospitali ya Hamburg, Ujerumani baada ya kusafirishwa kutoka SenegalPicha: picture-alliance/dpa

Uamuzi wa Air France umekuja siku moja baada ya Shirika la Ndege la Uingereza British Airways kusema kuwa linasitisha safari zake nchini Liberia na Sierra Leone hadi mwaka ujao kuhusiana na hofu ya ugonjwa wa Ebola.

Shirika la ndege la Ubelgiji, Brussels Airlines huwa na safari nne kwa wiki nchini Liberia na Sierra Leone na tatu nchini Guinea lakini pia limefuta huduma zake tangu Jumamosi iliyopita kutokana na kufungwa mpaka wa Senegal.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, David Nabarro aliyakosoa mashirika ya ndege yaliyositisha safari zake katika nchi hizo, akisema hatua ya kuendelea kuzitenga “inafanya iwe vigumu kwa Umoja wa Mataifa kufanya kazi yake”

Nabarro ambaye tayari amezuru Liberia, Sierra Leone na Guinea kama sehemu ya ziara yake katika nchi zilizoathirika na Ebola, kwa sasa yuko nchini Nigeria na amesema kuwa nchi zote zinapaswa kuwa kuchukua tahadhari kubwa kutokana na hali hiyo. "magonjwa hayaheshimu mipaka ya nchi. Yanasambaa bila mtu yeyote kuyadhibiti, na hivyo ina maana kuwa kama tunajaribu kupambana na mlipuko kama Ebola, lazima tuchukue hatua imara katika nchi zote zilizoathirika, kwa kushirikiana pamoja”.

Vogelgrippe Konferenz in Peking China David Nabarro
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, David NabarroPicha: AP

Mawaziri wa afya kutoka mataifa ya Afrika magharibi yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa ugonjwa huo wanakutana leo katika mji mkuu wa Ghana, Accra, kujadiliana kuhusu mbinu za kupambana na janga hilo.

Maafisa katika nchi hizo wanafanya juu chini kuudhibiti mlipuko wa virusi hivyo hatari ambao ni mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia. Kufikia sasa watu 1,400 wamepoteza maisha tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Wiki iliyopita, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilisema watu 13 waliuawa kutokana na dalili zisizojulikana za homa ya kuvuja damu, na kuwafanyia vipimo wengine kadhaa ambao waligusana na wahanga hao. Kisha ikathibitisha vosa viwili vya Ebola, lakini ikasema havihusiki na janga linaloendelea kuisakama Afrika Magharibi.

Wizara ya Afya ya Nigeria imeonya dhidi ya kuzembea katika vita dhidi ya Ebola, licha ya mgonjwa mmoja pekee kusalia hospitalini akitibiwa virusi hivyo na wengine saba wakiruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupona.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo