Hali ya COVID-19: Ujerumani iko mbioni kurejesha vizuizi
23 Novemba 2021Uholanzi imeanza kuwasafirisha wagonjwa wa COVID-19 hadi Ujerumani kupunguza shinikizo kwa hospitali za Uholanzi zinazojitahidi kushughulikia ongezeko la maambukizo ya virusi hivyo.
Takwimu kutoka Taasisi ya magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch nchini Ujerumani, zimeonesha kuwa viwango vya maambukizo katika muda wa siku saba vimeongezeka kufikia 399.8 kwa kila watu laki moja hii leo, hii ikiwa ni siku ya 16 mfululizo ambapo viwango hivyo vimekuwa vya juu mno.
Spahn amesema kuwa maeneo zaidi ya umma yanapaswa kuruhusiwa kuingia tu wale waliopata chanjo ama kupona katika siku za hivi karibuni na pia waliothibitishwa kutokuwa na maambukizo.
Wakati huo huo, mgonjwa mmoja leo asubuhi alisafirishwa kwa gari la kubebea wagonjwa kutoka mji wa Rotterdam nchini Uholanzi hadi katika hospitali moja mjini Bochum nchini Ujerumani na mwengine anatarajiwa kusafirishwa baadaye leo. Haya ni kwa mujibu wa mamlaka ya afya nchini Ujerumani.
Idadi ya wagonjwa wa COVID-19 katika hospitali nchini Uholanzi imeongezeka kufikia kiwango cha juu kabisa katika wiki za hivi karibuni tangu mwezi Mei na inatarajiwa kuongezeka zaidi.
Hospitali za Ujerumani kwa ujumla zina vitanda 20 vya wagonjwa wa COVID-19 kutoka Uholanzi baada ya kuwatibu wagonjwa kadhaa wakati wa mawimbi yaliyopita ya maambukizo hayo katika siku za nyuma.
Mipango ya serikali ya Uholanzi ya kuweka vikwazo zaidi dhidi ya virusi hivyo ilisababisha ghasia za siku tatu kuanzia siku ya Ijumaa na watu zaidi ya 170 kukamatwa katika miji kote nchini humo.Austria yaanza zuio jengine kupambana na COVID-19
Mipango hiyo inajumuisha kuruhusu tu watu waliopata chanjo ama kupona hivi karibuni kutokana na ugonjwa wa COVID-19 kuingia katika maeneo ya umma lakini bado haijakuwa wazi iwapo serikali itapata uungwaji mkono zaidi kwa mipango hiyo kuwa sheria.
Kufikia jana Jumatau, vitanda 470 kati ya 1050 vya wagonjwa mahututi nchini Uholanzi vilikuwa vinatumiwa na wagonjwa wa COVID-19 na hospitali tayari zimeanza kupunguza huduma za kawaida pamoja na matibabu ya saratani na upasuaji wa moyo.
Mbali na hayo, Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ilmewashauri raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Ujerumani na Denmark kwa sababu ya kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona katika mataifa hayo.
Hata hivyo, msemaji wa ikulu ya White House, Jen Psaki, amesema kuwa maafisa wa afya nchini humo hawajapendekeza hatua kali ama vizuizi vya kiuchumi kukabiliana na ongezeka la visa hivyo vya maambukizi.