Hali ya Covid-19 bado ni tete India
5 Mei 2021Watu 3,780 wamefariki nchini India katika muda wa saa 24 zilizopita. Ni idadi ya juu kabisa toka wimbi la pili la virusi vya corona kuikumba nchi hiyo. Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO limesema India pekee ilirekodi asilimia 46 ya jumla ya visa ulimwenguni na asilimia 25 ya jumla ya watu waliofariki mnamo wiki moja iliyopita.
Watu wengi walifariki kutokana na kukosa huduma ya oksijeni. Serikali ya Waziri Mkuu, Narendra Modi imelaumiwa kwa kutoshughulikia mapema janga hilo. Siku za nyuma India ilishuhudia mikusanyiko ya kidini na matamasha ya kitamaduni yaliyowakusanya maelfu ya watu.
Misaada ya kimataifa kwa India
Misaada ya kimataifa imepelekwa India ili kuwahudumia wagonjwa. Rais wa Marekani, Joe Biden amesema msaada zaidi wa nchi yake utapelekwa India.
''Tumeisaidia India kwa kiasi kikubwa. Nilizungumza na waziri Mkuu wa India Modi. Anachohitaji zaidi ni vifaa ili kutengeneza na kuhifadhi chanjo. Tumemtumia vifaa hivyo, tumemtumia oksijeni. Tumetuma vifaa vingi vya aina hiyo. Hivyo tunafanya mengi kwa ajili ya India'',alisema Biden.
Siku ya Jumanne, rais Biden alizindua hatua mpya ya chanjo ambayo itawajumuisha vijana wa miaka 12 na kuwalenga Wamarekani wanaokaidi kupewa chanjo. Biden amesema kuwa ifikapo Julai 4, asilimia sabini ya Wamarekani watakuwa wamepewa chanjo dhidi ya Covid-19. Zaidi ya watu milioni 145 tayari wamepewa angalau dozi moja ya chanjo nchini Marekani.
Umoja wa Ulaya wapongeza kampeni yake ya chanjo
Canada imeripoti leo kisa cha kwanza cha mtu aliyefariki kufuatia kuganda kwa damu baada ya kupewa chanjo ya AstraZeneca. Kwa jumla Canada iliripoti visa vitano vya kuganda kwa damu baada ya zaidi ya watu laki mbili na hamsini elfu kupewa chanjo ya AstraZeneca nchini humo. Hata hivyo, viongozi wanaelezea manufaa ya chanjo hiyo kuliko athari zake.
Barani Ulaya pia zoezi ya kutoa chanjo linaendelea. Halmashauri ya Kuu ya Umoja huo imepongeza hatua ya chanjo iliofikiwa hadi sasa ambako robo ya wananchi wa Ulaya tayari wamepewa chanjo. Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema ifikapo Julai asilimia 70 ya wananchi wa Ulaya watakuwa wamepewa chanjo dhidi ya Covid-19. Ujerumani imetangaza kulegeza masharti kwa watu waliopewa dozi zote mbili za chanjo ifikapo wiki ijayo.