Hali kisiwani Madagascar
23 Machi 2009
Maelfu ya wabuki wameandamana hii leo mjini Antananarivo dhidi ya kunyakua madaraka Andry Rajoelina na kudai rais aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasi Marc Ravalomanana arejee madarakani.Maandamano hayo yanautia hofu utawala ambao tokea hapo umedhoofishwa na uhasama wa jumuia ya kimataifa.
Waandamanaji hao wamehanikitza wakisema kwa kibuki "Avereno Dadanay,Avereno Ravalo"-waakimaanisha "mrejesheni baba ,mrejesheni Ravalomanana".
Waandamanaji hao waliopindukia elfu nane walipaza sauti kupinga pia kipindi cha mpito kilichoahidiwa na Rajoelina.
Maandamano hayo yamefanyika katika uwanja wa Ambohijatovo,kati kati ya mji mkuu Antananarivo,uwanja uliobadilishwa na Andry Rajoelina January 17 iliyopita na kuitwa "uwanja wa demokrasia" ,wakati alipokua bado kiongozi wa upande wa upinzani.
Wanaharakati zaidi ya elfu tatu walikusanyika hapo hapo ijumaa mosi iliyopita pia kumpinga meya huyo wa zamani wa Antananarivo.
"Tunaamini kuingia madarakani Andry Rajoelina ni kinyume na sheria na jumuia ya kimataifa inatuunga mkono" amesema hayo msemaji wa chama cha TIM cha Marc Ravalomanana- Andrianatoandro Raharinaivo.
"Tunataka Rajoelina atoke madarakani,Kisiwani Madagascar mtu haingii madarakani bila ya uchaguzi" amesema mwanaharakati mwengine ambae hakutaka jina lake litajwe.
Wabunge kadhaa walihutubia wakati wa mkutano wa hadhara ulioitishwa hii leo,jukwaa likipambwa kwa picha ya Marc Ravalomanana na mabango ya kampeni ya uchaguzi iliyompatia upya ushindi mnamo mwaka 2006.
Umati huo wa watu ulitawanyika leo mchana
wanaharakati wakiahidi kurejea tena kesho.
Makundi madogo madogo ya waandamanaji walielekea katika uwanja wa May 13-ngome ya wanaharakati wanaomuunga mkono Rajoelina.
Wimbi hili la malalamiko dhidi ya Rajoelina limechipuka katika wakati ambapo jumuia ya kimataifa imelaani vikali kuingia madarakani meya huyo wa zamani wa Antananarivo,kwa njia zinazotajwa kua " si za kidemokrasi" wengine wakiutaja utaratibu mzima kua "njama ya mapinduzi".
Umoja wa Afrika na wafadhili kadhaa wa Madagascar wameutaka utawala mpya kisiwani humo uheshimu katiba.
Na viongozi wa taifa na serikali za jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika-SADC wanatazamiwa kukutana March 30 ijayo kuzungumzia miongoni mwa mengineyo hatua kali dhidi ya utawala mpya wa Madagascar.Msemaji wa jumuia ya SADC,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Afrika kusini Ronnie Mamoepa anasema vikwazo vya kiuchumi navyo pia vitazingatiwa.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP Reuters
Mhariri:Abdul-Rahman Mohammed