Gündogan atafakari kuondoka Dortmund
11 Januari 2016Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye amekuwa katika klabu ya Dortmund tangu 2011, alidokeza mwaka jana kuwa angeondoka huku vilabu kadhaa nchini Italia na Premier League ya England vikimtaka, kabla ya kusaini mkataba mpya wa miaak miwili mwezi Julai.
Gündogan ameliambia gazeti la Bild leo kuwa hajafanya uamuzi wowote na lazima atathmini kila kitu kwa sababu urefu wa taaluma ya mtu una ukomo. Ameongeza kuwa kila kitu kingali wazi, na kuwa mkataba wake ujao utakuwa mrefu na sio wa mwaka mmoja tu. Dortmund kwa sasa wako katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Bundesliga.
Kiessling nusra aihame Leverkusen
Mshambuliaji wa zamani wa Ujerumani Stefan Kiessling alikuwa karibu kujiunga na Hanover katika kipindi hiki cha uhamisho, kabla ya kuamua kusalia katika Bayer Leverkusen.
Kiessling ameliambia gazeti la Bild leo kuwa nusra ahame baada ya kukasirishwa na sehemu ya kwanza ya msimu ambao mchezaji aliyesainiwa Javier “Chicharito” Hernandez aling'ara katika safu ya mashambulizi.
Anasema alikwenda Hanover, maana kulikuwa na ombi la kumtaka. Kiessling mwenye umri wa miaka 31 anamfahamu kocha wa Hanover Martin Bader kutoka klabu ya Nüremberg. Licha ya kutoanza mechi nyingi, Amefunga magoli matatu pekee katika Bundesliga, ikilinganishwa na 11 ya Hernandez. Amesema atafanya mazungumzo na uongozi wa Leverkusen mwishoni mwa msimu kabla ya kuchukua uamuzi wowote.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohamed Khelef