Guterres aonya Gaza inaendelea kuteseka 'kila baada ya saa'
29 Oktoba 2023Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo Jumapili ameonya kuwa hali katika Ukanda wa Gaza inayotawaliwa na Hamas inazidi kuzorota kwa kasi, huku akirudia ombi la kusitishwa kwa mapigano ili kukomesha kile alichokiita "jinamizi" la umwagaji damu.
Soma pia: Guterres atoa wito wa usitishwaji mapigano Gaza
Gutterres ameyasema hayo akiwa ziarani nchini Nepal na kuongeza kwamba badala ya kusimamisha mashambulizi hoja inayoungwa mkono na jumuiya ya Kimataifa, Israel imezidisha mashambulizi yake ya kijeshi.
Baada ya mashambulizi makubwa ya mabomu kwa majuma kadhaa katika Ukanda wa Gaza, wizara ya afya Palestina imesema watu zaidi 8,000 wameuwawa, huku jeshi la Israel likisema hatua ya pili ya vita imeanza kwa uvamizi wa ardhini tangu Ijumaa.