Guterres alaani mauaji ya watu 160 nchini Burkina Faso
6 Juni 2021
Vyanzo kutoka eneo yalikofanyika mashambulizi hayo, wanasema zaidi ya miili ya wahanga 160 imefukuliwa kutoka makaburi ya pamoja, 20 miongoni mwao wakiwa ni watoto.
Katika tangazo lake lililochapishwa Jumamosi jioni, Guterres amelaani shambulizi hilo ''la kuchukiza'', na kuitolea wito jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi katika kupiga vita vurugu zitokanazo na misimamo mikali.
Soma zaidi: Ufaransa na G5 kufanya mkutano wa kilele kuhusu uasi wa Sahel
Rais wa Burkina Faso Roch Marc Christian Kabore amesema shambulizi hilo lililotokea karibu na mpaka wa Mali na Niger, limefanywa na wanajihadi, na limewalenga raia na pia wanajeshi wa serikali.
''Majeruhi kadhaa wameaga dunia kutokana na majeraha waliyoyapata, na tumekuwa tukigundua miili mingine'', amesema Rais Kabole wakati idadi ya waliokufa ilipokuwa imekadiriwa kuwa 138.
Uvamizi wa usiku wa manane
Kulingana na walioshuhudia, shambulizi hilo lilianza saa nane usiku, likilenga kambi ya wafanyakazi wa msaada wa kujitolea wa shirika la VDP (Volunteers for the Defence of the Motherland), kabla ya kuenea katika makaazi ya raia.
Kiongozi wa upinzani nchini Burkina Faso Eddie Komboigo amesema ''mauaji ya halaiki dhidi ya watu wetu yanapaswa kusimama, bila masharti yoyote. Hatutatachoka kukumbusha kuwa kila hatua ichukuliwe kuwalinda watu wa Burkina Faso.''
Soma zaidi: Wanajeshi zaidi wa Mali wauawa
Serikali ilichapisha tangazo jioni ya Jumamosi, ikisema wanajeshi walikuwa wamepelekwa kwenye eneo yalikotokea mauaji hayo, ili kupambana na wanamgambo wavamizi.
Shambulizi hili baya la Jumamosi lilifanyika saa chache baada ya jingine lililotokea Ijumaa katika kijiji cha Tadaryat katika jimbo lile lile la Yagha. Mlinzi wa kujitolea alikuwa miongoni mwa waliouawa katika kijiji hicho.
Ukanda wa Sahel, ngome ya makundi ya jihadi
Hakuna taarifa kamili kuhusu kundi lililofanya mauaji hayo, wala sababu ya shambulizi lao. Hata hivyo, yapo makundi mengi yenye silaha katika Ukanda wa Sahel, ambao umeenea kati ya Bahari Nyekundu na Bahari ya Atlantiki.
Baadhi ya makundi hayo yametangaza utiifu kwa makundi ya kigaidi ya al-Qaida na lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS.
Ingawa Burkina Faso kwa muda mrefu haikusumbuliwa na makundi hayo, mashambulizi kwenye ardhi yake yamekuwa yakiongezeka tangu mwaka 2015.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa watu milioni 1.2 wamelazimika kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe. Watu wapatao 1,400 wameuawa katika kipindi cha miaka 6 iliyopita, hii ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu hizo za Umoja wa Mataifa.
afpe, dpae