1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUswisi

Gumzo la ushirikiano na Trump latawala Jukwaa la Uchumi

22 Januari 2025

Huku Jukwaa la Uchumi Duniani WEF likipamba moto huko Uswisi, Rais wa Marekani Donald Trump amempelekea kila mmoja kupata cha kuzungumzia, kutokana na hatua alizochukua katika siku yake ya kwanza aliporudi afisini.

https://p.dw.com/p/4pRnI
Schweiz Davos 2025 | EU-Kommissionspräsidentin von der Leyen bei Session auf Weltwirtschaftsforum
Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Baada ya kusaini agizo la kuiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba wa mazingira wa Paris wa mwaka 2015, viongozi wa Ulaya wakiongozwa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen wametetea suala la mabadiliko ya tabia nchi kutokea mwanzo wa mijadala katika jukwaa hilo.

Von der Leyen ameutaja mkataba wa Paris wa mwaka 2015kuwa "matumaini ya ubinadamu" na akaapa kwamba Ulaya itashirikiana na mataifa yote yanayotaka kuyalinda mazingira na kuzuia ongezeko la joto duniani.

Tehran kushirikiana na vyema na Marekani

Mbali na hayo masuala ya mazingira, waziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia aliyehudhuria kongamano hilo pia amesema haoni kama utawala mpya wa Rais Trump ukiongeza hatari ya mzozo kati ya Israel na Iran, suala ambalo kanda ya Mashariki ya Kati imekuwa ikihofia tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza.

Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al-Saud amesema pia kwamba anatarajia kwamba mkondo atakaouchukua Donald Trump kwa Iran utapokelewa kwa nia njema na Tehran kwa ajili ya kushirikiana na Marekani.

Naye Rais wa Israel Isaac Herzog katika jukwaa hilo hilo la uchumi duniani, ametoa wito kwa juhudi za ulimwengu kupambana na ugaidi. Herzog amesema ugaidi unasababisha maafa maeneo kama Afrika na maeneo mengine duniani.

Rais huyo wa Israel vile vile amerudia mara kadhaa hatari inayotokana na Iran na makundi inayoyaunga mkono. Herzog amesema chanzo cha maovu ni ugaidi na hasa ugaidi unaochochewa na Iran.

Ama kuhusiana na vita vya Urusi nchini Ukraine, Rais Volodymyr Zelenskiy ambaye anatafuta kukutana na Rais Donald Trump, amesema kutahitajika angalau walinda amani laki mbili wa Ulaya ili kuzuia shambulizi jengine la Urusi, endapo kutapatikana makubaliano yoyote ya kusitisha vita.

Rais wa Ukraine Volodymyr zelenskiy akiwa Davos
Rais wa Ukraine Volodymyr zelenskiy akiwa DavosPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Katika hotuba mbele ya jukwaa hilo la kiuchumi duniani, Zelenskiy amesema anatumai kwamba Trump atavimaliza vita hivyo dhidi ya nchi yake kwa njia ya busara. Rais huyo wa Ukraine amesema Trump alimwambia kwamba atafanya kila jitihada kuvimaliza vita hivyo mwaka huu. Lakini Zelenskiy anadai kupatikana kwa amani ya kudumu ni muhimu kuliko usitishwaji wa haraka wa vita.

Na katika hotuba yake huko Davos, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza kuendelea kwa ushirikiano wa karibu kati ya Ujerumani na Marekani ila akadai ni muhimu kusiwepo pia na ujanja wa aina yoyote ile kutoka kwa Trump.

Scholz amesema ushirikiano kati ya nchini marafiki Ulaya na Marekani ni muhimu kwa ajili ya amani na usalama kote duniani na ndicho kichocheo cha ustawi wa kiuchumi pia.

Trump kuwa mshirika muhimu kwa Ulaya

Naye Friedrich Merz, kiongozi wa upinzani nchini Ujerumani kutoka chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union CDU ambaye ndiye anayeongeza tafiti za maoni za Kansela ajaye wa Ujerumani, amehudhuria juklwaa hilo la kiuchumi pia na ameelezea matumini kuhusiana na ushirikiano wa Ulaya na Donald Trump.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akilihutubia Jukwaa la Uchumi la Davos
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akilihutubia Jukwaa la Uchumi la DavosPicha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Merz wakati alipokuwa akizungumza na Rais wa jukwaa hilo la kiuchumi Borge Brende amesema anahisi kuwa Trump atakuwa mshirika muhimu kwa Ulaya na kwamba misimamo yake kwa kawaida hujulikana, kwa hiyo la muhimu ni kutambua pale misimamo yao inapooana.

Merz pia amesema atashirikiana zaidi na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni endapo atakuwa Kansela, kwani anahisi ni kiongozi anayeuunga mkono Umoja wa Ulaya.

Wakati huo huo nguli wa kandanda wa Uingereza David Beckham amehudhuria jukwaa hilo la kiuchumi kwa mara ya kwanza na amewataka viongozi wa dunia kuhakikisha kwamba wasichana wanapata nafasi sawa na wavulana.

Beckham ameapa kuawahamasisha wasichana kama sehemu ya mpango wa kuwasaidia watoto kote duniani.

Vyanzo: APE/AFPE/DPAE/Reuters