1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghuba: Corona yaongeza hali mbaya kwa wafanyikazi wageni

4 Mei 2020

Wafanyakazi kutoka nchi za nje wamo katika mashaka makubwa ya kulipwa mishahara ya chini na kudhulumiwa katika nchi za Ghuba kutokana na athari zilizosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3bjPG
VAE Dubai | Arbeiter
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Jebreili

Wakati janga la corona linakwamisha shughuli za kiuchumi duniani kote, kusimama kwa shughuli za biashara kunawaumiza zaidi wafanyakazi wa vipato vya chini katika nchi za Ghuba na hasa wale wanaotoka nchi za nje.

Serikali za Saudi Arabia na Bahrain zimeahidi kuwasaidia wafanyakazi wazaliwa lakini wageni wameachwa patupu. Umoja wa Falme za Kiarabu umebadilisha sheria na hivyo kuziruhusu kampuni kuvunja mikataba ya kazi ya wafanyakazi wageni. Mabadiliko hayo yatawaruhusu waajiri kuibadilisha mikataba ya kazi, kupunguza ujira na kuwalazimisha wageni hao kuchukua likizo bila ya malipo.

Wiki iliyopita Benki ya dunia ilisema kusimama kwa shughuli za kiuchumi duniani kutokana na janga la COVID -19 kumesabisha kupungua sana kwa fedha ambazo wafanyakazi wageni wanatuma nyumbani kwa ajili ya familia zao. Wafanyakazi wageni wanaolazimishwa kubakia pale walipo huwamo katika hali zinazohatarisha afya zao kutokana na mazingira mabaya yanayowakabili.

Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani
Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al ThaniPicha: Getty Images/S. Gallup

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametanabahisha juu ya hatari inayotokana na watu hao kujazana katika nyumba, kiasi kwamba inakuwa vigumu kwao kuzingatia utaratibu wa kuweka umbali wa mita mbili kati ya mtu na mtu.

Hali ni mbaya zaidi kwa wafanyakazi wageni wanaojenga sehemu zitakazotumiwa wakati wa mashindano ya kombe la dunia yanayotarajiwa kufanyika mnamo mwaka 2022. Wageni kumi wanawekwa katika chumba kimoja bila ya maji ya bomba na katika mazingira ya uchafu.  

Mbali na mazingira mabaya ya kazi, yanayowawakabili wafanyakazi wageni, watu hao sasa wanabaguliwa na wale wanaofanya kazi za utumishi wa majumbani wanafanyiwa dhulma. Sasa hawaruhusiwi kutoka nje ya nyumba wanakofanya kazi.

Shirika la kueteta haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa mwito kwa Qatar wa kulinda maslahi ya wafanyakazi wageni kama ilivyoahidi. Shirika hilo limesema haki hizo zinapaswa kutekelezwa sasa zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwa manufaa ya watu hao waliotoa mchango katika kuujenga uchumi wa Qatar.

Chanzo:/ LINK: http://www.dw.com/a-53297391