1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia zaongezeka Syria

19 Septemba 2016

Makubaliano ya kusitisha vita nchini Syria yamesambaratika. Hii ni baada ya mashambulizi yanayoongozwa na Marekani kuwauwa wanajeshi wa serikali katika shambulizi la kwanza la angani kwa muda wa wiki moja mjini Aleppo.

https://p.dw.com/p/1K4oH
Syrien Luftangriff auf Aleppo
Raia wa Syria wanaagalia vifusi kufuatia shambulizi la angani la muungano ulioongozwa na Marekani tarehe 18 mwezi Septemba.Picha: Getty Images/AFP/K. Al-Masri

Msururu wa mashambulizi katika ngome za waasi mjini Aleppo hapo jana , unahatarisha kuzuka kwa mapigano mapya mjini humo na huenda ukasababisha kitisho kikubwa katika makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa kati ya Marekani na Urusi .

Kusitishwa kwa mapigano mjini Aleppo na kupelekwa kwa msaada wa kibinadamu unaohitajika kwa dharura mjini humo yalikuwa maswala makuu ya mkataba ulioafikiwa Jumatatu iliyopita.

Wadhamini wa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yaani serikali za Urusi na Marekani, zimelaumiana na uhusiano kati nchi hizo mbili kuonekana kusambaratika zaidi baada ya mashambulizi hayo ya Marekani yaliosababisha vifo vya wanajeshi wengi siku ya Jumamosi.

Kulingana na balozi wa Syria katika Umoja wa mataifa Bashar Jaafari, lengo la uchokozi huu wa Marekani ni kusababisha kusambaratika kwa mkataba huo .

Kundi linalofuatilia haki za kibinadamu nchini Syria lilisema Jana ilikuwa siku mbaya zaidi kufikia sasa ya makubaliano hayo ya kusitisha vita huku raia 11 wakiuawa katika maeneo ambayo vita vilipaswa kusitishwa.

Haya yanajiri huku malori 20 ya msaada yanayohitajika kufika Mashariki mwa Allepo na bidhaa za kutosha kuwalisha maelfu ya watu yakiwa bado yamekwama nchini Uturuki. Hii ni kulingana na afisa mkuu wa shirika la msaada la Umoja wa mataifa aliyesema haya hii leo saa kadhaa baada ya kukamilika kwa kipindi cha siku saba cha kusitisha mapigano nchini Syria .

Syrien Luftangriff auf Aleppo
Raia wa Syria watembea juu ya vifusi kufuatia shambulizi la angani dhidi ya ngome za waasi huko Karm al-Jabal .Picha: Getty Images/AFP/K. Al-Masri

Umoja wa mataifa unasema kuwa haujapata ruhusa inayohitajika na hakikisho la usalama la maafisa wake kutoka kwa serikali ya Syria kuendelea na safari yake ya kupeleka msaada katika mji wa Aleppo na maeneo mengine yasioweza kufikiwa. Yamkinika kuwa msaada huo umekwama katika eneo la mpaka huo kwa wiki moja sasa.

Takriban watu elfu 275 wamekwama katika eneo hilo la Aleppo bila ya chakula, maji , huduma za afya na mahala pa kuishi. Msururu huo wa malorei ndio wa kwanza uliobeba unga na bidhaa nyingine za chakula za kutosha kulisha watu elfu 185 kwa mwezi mmoja.

Msaada wa kibinadamu mjini Aleppo unatatizwa na vizuizi vya barabara ya kuingia katika ngome ya waasi katika mji huo ambayo baadhi ya sehemu zake zinathibitiwa na serikali na nyingine zikithibitiwa na waasi ambao wamekuwa wakisababisha vita vya mara kwa mara vya zaidi ya miaka mitano vya kutaka kuipindua serikali ya rais Bashar al- Assad.

Katika taarifa, Stephen Obrien , katibu wa shirika la msaada la umoja wa mataifa, alisema kuwa anatumaini kuwa pande zote mbili watakuwa na busara ya kuona kuwa msaada huo ni fursa ya kuleta mabadiliko na kusonga mbele na kwamba unapaswa kuchukuliwa kama hatua huru isiyokuwa na mwingilio wowote wa kisiasa au kijeshi.

Mwandishi: Tatu Karema

Mhariri: Yusuf Saumu