Ghasia zaendelea Ufaransa
1 Julai 2023Zaidi ya watu 1,300 wamekamatwa, licha ya ulinzi mkali na kufungwa kwa huduma za usafiri wa umma. Hayo yanajiri wakati marafiki na familia wakifanya maziko ya kijana huyo Jumamosi.
Waziri wa mambo ya ndani Gérald Darmanin amewaambia waandishi wa habari mapema Jumamosi kuwa licha ya matukio ya uporaji, uharibifu wa mali na makabiliano na polisi, vurugu zimepungua ikilinganishwa na Alhamisi usiku. Darmanin amesema zaidi ya magari 1,350 yamechomwa moto na kuna idadi ya visa 2,560 vya moto ulioanzishwa kwenye barabara za umma.
Soma zaidi: Hamkani bado si shwari Ufaransa kufuatia kifo cha Nahel
Uharibifu umeshuhudiwa zaidi Paris, Marseille, Lyon, na hata maeneo yaliyo chini ya utawala wa Ufaransa, nje ya taifa hilo ambapo kwa upande wa Guiana, mwanamume wa miaka 54 ameuwawa baada ya kupigwa risasi.
Mamlaka za Ufaransa zimesema takribani maafisa wa polisi 150 wamejeruhiwa wakati wa ghasia za Ijumaa usiku. Vikosi maalumu ni kati ya maafisa usalama 45,000, waliosambazwa kudhibiti maandamano.
Ili kukomesha vurugu, waziri wamambo ya ndani, Darmanin alisimamisha safari za mabasi na treni kote nchini humo kuanzia saa tatu usiku, hadi itakapotangazwa tena.
Waendesha mashtaka walianzisha uchunguzi rasmi wa mauaji ya bila kukusudia dhidi ya afisa wa polisi anayedaiwa kuwa alimfyatulia risasi kijana huyo aliyejulikana kwa jina la Nahel huko Nanterre.
Macron aahirisha ziara yake Ujerumani kushughulikia vurugu
Katika hatua nyingine, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameahirisha ziara yake nchini Ujerumani ili kushughulikia vurugu zinazoendelea nchini mwake kwa usiku wa nne mfululizo.
Ofisi ya rais wa Ujerumani imetangaza kuwa Macron amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na kumfahamisha kuhusu hali nchini mwake, wakati akiomba ziara yake iliyopangwa kuanza Jumapili iahirishwe.
Mapema Ijumaa Rais Macron, aliitisha kikao cha dharura kufuatia vurugu zilizojitokeza. Kinyume na ilivyotarajiwa na wengi, Macron hakutangaza hali ya dharura lakini alitoa wito kwa wazazi kuwaasa vijana wao wasishiriki kwenye maandamano ya vurugu
Timu ya soka ya Ufaransa imetoa wito wa kukomeshwa kwa machafuko. Katika kauli ya hiyo wachezaji wamesema kuwa vurugu hazitatui tatizo lolote na kwamba kuna njia nyingine za amani za watu kuonesha hisia zao. Timu hiyo imesema ni wakati wa kuomboleza, na kufanya mazungumzo
Mama wa kijana Nahel aliyeuwawa aliyejitambulisha kwa jina la Mounia M. ambaye familia yake ina asili ya Algeria, alikiambia kituo cha televisheni cha France 5 kuwa ana hasira na afisa wa polisi aliyemuua mwanaye lakini si kwa jeshi zima.