GENEVA : Yaelezwa bila ya maji hakuna uhai
22 Machi 2005Katika kuadhimisha Siku ya Maji Dunaini leo hii kiongozi anayeshughulikia masuala ya haki za binaadamu na misaada ya kiutu katika serikali ya Ujerumani Tom Keonigs amesema bila ya maji hakuna uhai.
Akizungumza katika kikao cha Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesema watoto wanakufa kila siku duniani kote kwa magonjwa yanayosababishwa na uhaba wa maji safi na uchafuzi wa maji hayo.
Ameongeza kusema wanawake inabidi wasafiri masafa marefu kuchota maji na wasichana ambao hubeba mitungi ya maji ndio watakaoathirika zaidi na kuwa watu wasiojuwa kusoma na kuandika hapo kesho.
Keonigs amesema kupata maji safi ni haki ya binaadamu ambayo hunyimwa watu bilioni moja kila siku na ni kwa ajili hiyo serikali ya Ujerumani imeliweka mbele suala la maji katika kikao cha hivi sasa cha Tume ya Haki za Binaadamu.