GENEVA : Uwekezaji wa kigeni haukusaidia sana Afrika
13 Septemba 2005Shirika la Umoja wa Mataifa linasema Afrika imenufaika kidogo kutokana uwekezaji wa kigeni unaonekana kuwa chachu ya maendeleo na yumkini hata ikashindwa wakati nchi zinazoendelea zikiwa kwenye ushindani wa kuvutia uwekezaji wa makampuni ya kigeni.
Makampuni ya kigeni yamemimina mabilioni ya dola kwenye sekta za mafuta na migodi barani Afrika lakini sekta hizo zimetowa faida chache katika fani ya kuongeza ajira au utajiri wa ndani ya nchi.Hayo yamebainishwa na repoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo UNCTAD.
Kwa mujibu wa shirika hilo uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja umeongezeka mara tisa zaidi kutoka miaka ya 1980 hadi mwaka 2004 na kufikia dola bilioni 18 kwa mwaka kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya dunia ya mafuta na madini.
Katibu Mkuu wa UNCTAD Supachai Panitchpakdi amewaambia waandishi wa habari kwamba mategemeo ya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni kuinuwa uchumi, kutanuwa biashara kueneza teknolojia na kuongeza ajira hayakufanikiwa kikamilifu kama ilivyotarajiwa.
Uchunguzi wa repoti hiyo umezitaja Ghana na Tanzania kuwa zimepokea kama asilimia 5 tu ya thamani ya dhahabu iliosafirishwa nje kutokana na uwekezaji wa kigeni.