GENEVA : Ujerumani yakaribisha mapendekezo ya Annan
22 Machi 2005Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Yoschka Fischer ameyakaribisha mapendekezo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kukifanyia mageuzi makubwa chombo hicho kwa kusema kuwa ni muhimu kwa amani na utengamano katika karne ya 21.
Akiwasili mjini Geneva kwa mkutano wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa ameyafananisha mapendekezo hayo na dawa ya afya yenye kuzingatia hali halisi ya mambo.
Ujerumani inawania kiti cha kudumu katika mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na imezinduwa kampeni ya pamoja na mataifa mengine matatu Japani,Brazil na India kuwania viti hivyo.
GENEVA : Yaelezwa bila ya maji hakuna uhai
Katika kuadhimisha Siku ya Maji Dunaini leo hii kiongozi anayeshughulikia masuala ya haki za binaadamu na misaada ya kiutu katika serikali ya Ujerumani Tom Keonigs amesema bila ya maji hakuna uhai.
Akizungumza katika kikao cha Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesema watoto wanakufa kila siku duniani kote kwa magonjwa yanayosababishwa na uhaba wa maji safi na uchafuzi wa maji hayo.
Ameongeza kusema wanawake inabidi wasafiri masafa marefu kuchota maji na wasichana ambao hubeba mitungi ya maji ndio watakaoathirika zaidi na kuwa watu wasiojuwa kusoma na kuandika hapo kesho.
Keonigs amesema kupata maji safi ni haki ya binaadamu ambayo hunyimwa watu bilioni moja kila siku na ni kwa ajili hiyo serikali ya Ujerumani imeliweka mbele suala la maji katika kikao cha hivi sasa cha Tume ya Haki za Binaadamu.