GENEVA : Burma yashutumiwa kwa dhuluma za raia
29 Juni 2007Kamati ya Kimataifa ya chama cha Msalaba Mwekundu ICRC imeishutumu serikali ya kijeshi ya Burma kwa kufanya dhuluma kubwa dhidi ya raia na mahabusu.
Imesema serikali ya Burma inawalazimisha maelfu ya mahabusu kutumika kama wapagazi kwa wanajeshi na kuwaweka kwenye hatari ya mapigano miongoni mwa hatari nyenginezo. Taarifa yao pia imetaja dhuluma za mara kwa mara zinazofanywa na jeshi dhidi ya watu na watoto wao wanaoishi kwenye mpaka wa Burma na Thailand kwa kuteketeza ugavi wao wa chakula.
Hatua ya kamati hiyo ya Msalaba Mwekundu sio ya kawaida kwani kwa kawaida hutowa malalamiko ya aina hiyo katika majadiliano ya siri.
Rais wa ICRC Jakob Kellenberger amesema mara kwa mara wamekuwa wakiilalamikia serikali ya Burma juu ya dhuluma hizo lakini serikali imeshindwa kukomesha dhuluma hizo.