G77 yahitimisha mkutano wake Kampala
22 Januari 2024Mkutano wa G77 hufanyika kila mwaka kuwezesha mataifa yanayoendelea hasa ya kusini mwa dunia kujadili njia za kushirikiana zaidi kibiashara na pia kuwa na sauti ya pamoja katika utungaji wa sera za kimataifa kuhusiana na biashara, uwekezaji na upatikanaji wa mtaji.
Lengo ni kujikwamua kutoka minyororo ya utegemezi wa misaada ya maendeleo ambayo huandamana na masharti makali kutoka kwa mataifa tajiri wafadhili.
Ni kwa msingi huu ndipo Katibu Mkuu wa Umoja Mataifa Antonio Guterres ameibua wazo kwamba taasisi za kifedha za kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) zichunguze upya mifumo ya utoaji mikopo kwa mataifa yanayoendelea.
Soma zaidi: Kundi la G77+China lataka mageuzi mfumo wa ulimwengu
"Benki zinazotoa fedha zinatakiwa kupewa mitaji ya kutosha na zibadili mifumo yao ya mikopo kwa mataifa yanayoendelea ili yaweze kuekeza katika mipango ya malengo endelevu ya maendeleo na yalegeze masharti ya kulipa madeni." Alisema Guterres.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa aliahidi kuwa katika mkutano utakaofanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mwezi Septemba utaweka wazi mikakati ya kubadili sera za mifumo ya mikopo na ulipaji madeni.
Jukwaa la 80% ya watu ulimwenguni
Mwaka 1964, mataifa 77 yalisaini mkataba wa kubuni jukwaa hilo ambalo sasa lina mataifa wanachama 134 yakiwa na jumla ya asilimia 80 ya idadi ya watu wote duniani.
Kwa sasa mataifa hayo yamekumbwa na mashaka na misukosuko ya kiuchumi, kijamii, mazingira na vita na ukosefu wa utabiti. hali inayotatiza juhudi za kufanikisha maazimio ya G77.
Soma zaidi: Nchi maskini zimeanza kulalamika Copenhagen
Akiufunga rasmi mkutano huo siku ya Jumatatu (Januari 22), mwenyekiti mpya wa G77, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alitaka kuendelea kuwepo ushirikiano baina ya kundi hilo la China ili "kuhakikisha kwamba kunakuwa na muundo wa kimataifa ambao unazingatia usawa kwa wote, kwani tunazidi kushuhudia tishio kwa mashirikiano miongoni mwa mataifa ambapo nchi zinatanguliza maslahi binafsi."
Mkutano huo aidha umeyataka mataifa ya Magharibi kutotumia kile wanachokitaja kuwa ukiukaji wa haki za binaadamu katika mataifa yanayoendelea kama kisingizio cha kuyanyima mikopo.
Miongoni mwa maazimio ni kuimarisha ushirikiano katika masuala ya uhamiaji ili kurahisisha shughuli za uwekezaji na biashara na, hivyo, hata gharama za kuendesha biashara zitashuka.