G20:Ghasia mitaani joto la kisiasa kwa Merkel
8 Julai 2017Gazeti la Kijerumani Bild linalotoka kila siku lilizungumzia kulaani kwake machafuko yalioshuhudia wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kushoto, wakiyawasha moto magari kadhaa, ku kutwaa ngawira madukani na kupambana na polisi wa kuzuwia fujo kwa mawe na chupa. Gazeti hilo katika toleo la leo liliandika; mtu anaweza kuyaita matukio ya Hamburg kama ni kushindwa kwa dola kuidhibiti hali ya mambo kwa saa 48 na mkutano huo wa kilele kugeuka uwanja wa mapambano. Bila shaka polisi walijitahidi kufanya kila wawezelo lakini mitaa ilidhibitiwa na magenge ya wafanya fujo.
Malalamiko na ukosoaji mkubwa ulitolewa pale polisi 20,000 katika mji huo alikozaliwa Kansela Angela Merkel ulipoingia katika siku ya tatu ya vurugu kupinga mkutano huo wa G20, ambapo aliwakaribisha rais Donald Trump wa Marekani, Vladimir Putin wa Urusi na viongozi wengine wa dunia. Eneo la mkutano wao ulifanyika kukiwa na ulinzi mkali, lilizungukwa na vizuizi vya barabarani vilivyowekwa na polisi, maduka yalioharibiwa na chupa na vigae vilivyozagaa kila mahali baada ya usiku wa vurumai, huku polisi waliokuwa na silaha wakiwatia nguvuni wanaharakati , waliokuwa wakiwatupia mawe kutoka kwenye sakafu za majengo ya karibu. Kwa mtazamo wa mazingira yaliokuweko wa jarida la Bild , Ujumbe mahsusi kutoka Jiji la Hamburg ulikuwa, Magenge ya wafanya fujo yakitaka kutawala hutawala.
Polisi mmoja alimlaumu kansela Merkel na Meya wa Hamburg Olaf Scholz kwa kuruhusu hali hiyo ijitokeze, ambapo zaidi ya polisi 200 na idadi isiyojulikana ya waandamanaji walijeruhiwa, na hasa wakalaumiwa kwa kuuchagua mji huo kuwa kituo cha mkutano wa kilele wa G20.
Kuchaguliwa kwa Hamburg
Kwa muda mrefu serikali ya Merkel imesisitiza kwamba kuuchagua mji huo kuwa mahala pa mkutano wa kilele wa G20, kumetokana na mji huo kujitambulisha kama mji wa mchanganyiko wa watu wa tamaduni mbali mbali na" mlango wa kuelekea kwengineko duniani." Hoja nyengine ni kwamba kinyume na miaka ya nyuma ambapo viongozi wamekuwa wakijifungia maeneo ya vijijini, kukutana kwao katika mji huo mkubwa kungeonesha kuwa hawajitengi na umma.
Kumefanyika takriban mikutano ya hadhara 30 kupinga mkusanyiko huo wa viongozi wa G20, kuanzia maandamano ya amani na karamu za barabarani zikiandamana na muziki, hadi vizuizi barabarani na upinzani kwa kutumia mashua baharini na machafuko baada ya usiku kuingia.
Akitetea hatua zote hizo, Jana Schmeider kutoka muungano wa wanaopinga mkutano wa G20, amesema kuwa mitaani ni sehemu ya waandamaji na sio mkutano wa kilele. Gazeti la Spiegel katika matandao wake lilisema bibi Merkel ambaye anakabiliwa na uchaguzi mkuu Septemba 24, anapaswa kutambuwa kitakachokumbukwa zaidi ni picha za magari yanayowaka moto na wanaharakati wenye msimamo mkali na sio mkutano wa kilele wa G20.
Baada ya siku mbili za mapambano makali na waandamanaji, polisi mjini Hamburg wameanza kazi ya kulisafisha eneo la karibu na mkutano huo wa G20.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp,dpa
Mhariri: Daniel Gakuba