Filamu ya Joseph Kony yasambazwa
9 Machi 2012Filamu hiyo ya dakika 30 ilisambazwa kote kwa kutumia mtandao wa twitter ikiwa na jina Kony 2012 na Stop Kony.
Jana pekee filamu hiyo ilikuwa imeshatizamwa mara millioni 40, na katika mtandao wa kijamii wa Twitter habari hiyo ndio iliokuwa nambari moja dunia nzima kutokana na watu kuzungumzia video hiyo mara kwa mara.
Wasanii mashuhuri kama vile George Clooney, Rihanna, Justin Bieber na Oprah, waliunga mkono filamu hiyo inayoshinikiza kukamatwa kwa kiongozi huyo wa waasi.
Kampeni ya kushinikiza kukamatwa kwa Joseph Kony, iliopelekea kutengenezwa kwa filamu hiyo iliongozwa na mtengenezaji filamu Jason Russell kutoka Invisible children mjini San Diego Mexico. Kabla ya kutengenezwa kwa filamu hiyo Russell alikuwa ametembelea kaskazini mwa Uganda.
Kundi la Invisible Children limesema lilitengeneza filamu hiyo ili Joseph Kony kiongozi wa kundi la waasi la Lord's Resistance akamatwe kwa haraka na kuhukumiwa kwa makosa alioyafanya. Kony anajulikana sana kwa kuwateka nyara watoto na kuwalazimisha kushiriki katika vita.
Russell aliyemshirikisha mtoto wake wa kiume katika filamu hiyo na pia watoto wa Uganda sasa amewataka watazamaji kuwashinikiza maafisa wa serikali kukubali kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Uganda.
Joseph Kony pamoja na washirika wake wa karibu waliwekewa vibali vya kukamatwa na mahakama ya ICC hapo mwaka 2005.
Hata hivyo filamu hiyo imekosolewa kwa kutoa habari zinazopotosha juu ya jinsi mambo yalivyo, hasaa sasa ambapo kiongozi huyo wa LRA anaaminika kutoroka Uganda na kukimbia kusini mwa Sudan ama Jamhuri ya Afrika ya kati.
Serikali ya Uganda imesema inashukuru kwa jitihada zilizofanywa kwa kutengenezwa filamu hiyo na kwamba jeshi la Marekani tayari lipo nchini humo kusaidia katika kumsaka Kony.
Lakini Marekani kupitia msemaji wake Victoria Nuland imekana kwamba inachukua jukumu zaidi katika mapambanao dhidi ya kundi la waasi wa LRA.
Mwandishi: Amina Abubakar/RTRE
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman