FIFA Conf. Cup Ujerumani kuumana na Chile
2 Julai 2017Urusi imesifiwa jana Jumamosi kwa kufanikisha kwa mafanikio mashindano hayo ya kombe la mabara , ikiwa ni kujipasha moto kwa ajili ya fainali za kombe la dunia , licha ya kwamba nchi hiyo imekabiliwa na maswali mapya juu ya suala la matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli, yaani doping.
Nahodha wa Ujerumani Julian Draxler alijiunga na rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Gianni Infantino katika kuishukuru Urusi kabla ya fainali ya leo. "Ahsante kwa maandalizi yenu mazuri, kwa kuwa na watu wengi wa usaidizi wakati wote wa mashindano, na kwa kila wakati ambapo mmetufanya tujisikie salama," Draxler amesema katika taarifa iliyochapishwa Jumamosi na timu ya Ujerumani.
Infantino alisema baadaye katika mkutano na waandishi habari katika uwanja wa mpira wa mjini St.Petersburg kwamba "kila kitu kilienda vizuri," Urusi. Tulikuwa tunasikia kuhusiana na ghasia , kuhusu matukio, kuhusu wahuni michezoni , kuhusu ubaguzi, lakini hatukuwa na kitu chochote," Infantino alisema, akimaanisha maswali ya kabla ya michezo hiyo ambayo yalihusishwa na kandanda katika taifa hilo mwenyeji.
Pamoja na hayo kivuli cha doping kilichoko katika michezo nchini Urusi kutokana na wimbi la ripoti za shirika linalopambana na matumizi ya madawa hayo katika michezo duniani tangu mwaka 2015 pia zimejitokeza wakati wa michuano hiyo ya kupasha mwili joto ya wiki mbili kabla ya kombe la dunia.
Urusi na doping
FIFA inafahamu kuhusu sampuli 155 za watuhumiwa zilizotolewa na wachezaji nchini Urusi ambazo zinahitaji kufanyiwa uchunguzi, mtaalamu wa WADA aliyeteuliwa kuchunguza Richard McLaren amekiambia kitu cha televisheni nchini Ujerumani ARD.
Infantino , ambaye aliongozana na naibu waziri mkuu wa Urusi Vitaly Mutko, alisema jana Jumamosi hawezi kupanga muda maalum kwa kesi hizo za Urusi ambazo kamati ya nidhamu ya FIFA inapaswa kutekeleza kutokana na ripoti za McLaren.
Hata hivyo, maamuzi muhimu kuhusiana na madai ya profesa huyo kutoka Canada wa masuala ya sheria dhidi ya Urusi yanakaribia na yanaweza kutangazwa katika muda wa wiki chache zijazo.
Jopo la kimataifa la kamati ya Olimpiki inajitayarisha kutangaza matokeo ya hukumu yake ya mwanzo inayohusu wanamichezo wa Urusi katika michezo ya majira ya baridi mwaka 2014 ambao wanashukiwa kunufaika na njama za doping zilizoungwa na serikali katika maabara ya Olimpiki mjini Sochi.
"Tunasubiri pia ripoti hizo," Infantino alikiri Jumamosi. Mutko, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kombe la dunia mwaka 2018 na alihusishwa katika ushahidi wa McLaren kuficha kesi moja ya doping katika kandanda, kwa mara nyingine tena alikanusha vikali madai kwamba serikali ilikuwa inaendesha mpango huo wa doping.
Rais wa Urusi Vladmir Putin hana mpango wa kuhudhuria fainali ya kombe la mabara leo mjini St.Petersburg zimeeleza duru za FIFA. Putin alihudhuria mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo mjini St. Petersburg hapo Juni 17 wakati aliposhuhudia mchezo kati ya Urusi na New zealand akiwa pamoja na rais wa FIFA Giovanni Infanitino.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / ape
Mhariri: Sylvia Mwehozi