FC Kolon yachungulia daraja la pili
23 Aprili 2018Schalke 04 imeweka mguu mmoja katika michuano ya Champions League msimu ujao wakati FC Kolon iko katika ukingo wa kushuka daraja baada ya sare ya mabo 2-2 jana Jumapili. Wachezaji pamoja na mashabiki wa FC Kolon macho yalimiminika machozi kuiona timu yao ikiporomoja licha ya kufanya juhudi za ziada kwa kupata ushindi muhimu jana.
Kolon walihitaji kupata ushindi jana ili kuweka hai matumaini yao ya kubakia katika daraja la kwanza lakini mabao ya haraka haraka mnamo kipindi cha kwanza ya Breel Embolo na Yevhen Konoplyanka yakiwakatisha tamaa , licha ya kupigana kufa na kupona na kukomboa mabao hayoMarcel Risse ndie aliyefunga bao la kukomboa la FC Kolon jana.
"Nashukuru sana , wakati nikiona , mashabiki wanavyotaka tupambane tu kwenda mbele, licha ya kwamba hisia zinatuambia hakuna matumaini na hata hivyo wanaikubali hali, wakati tumetoka sare tu ya mabao 2-2 dhidi ya Schalke. Pamoja na hayo inaumiza sana, kuona mashabiki jinsi walivyovunjika moyo na kuumia. Hisia kama hizo zinatupata sisi kama wachezaji katika hali kama hiyo uwanjani."
Mchezo wa jana ulikuwa muhimu kwa timu zote Schalke pamoja na FC Kolon kwa kuwa Schalke ilihitaji kujiimarisha katika nafasi yake kama makamu bingwa msimu huu ikiifuata Bayern Munich ambacho ilikwisha nyakua ubingwa wa Bundesliga. Schalke hata hivyo iko na mwanya wa pointi pointi mbili ikipishana na hasimu wake mkubwa Borussia Dortmund ambayo ilifanya maajabu siku ya Jumamosi jioni kwa kuikandika Bayer Leverkusen kwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza mwaka huu kufanya vizuri zaidi, kama anavyosema kocha wa Dortmud Peter Stoeger.
"Mpinzani wetu alikuwa muhimu, na tulipata pointi 3. Inatusaidia, bila shaka, wengine wanapaswa kutukimbilia. Lakini ulikuwa mchezo wa pointi muhimu , kwasababu iwapo ungemalizika kwa sisi kushindwa , moto ungewaka, licha ya kuwa tumo katika eneo la nafasi za kucheza katika Champions League. lakini kungekewa na maswali mengi , kama ilivyokuwa huko nyuma."
Hamburg SV nayo imo katika mchakato wa kujinasua kutoka kushuka daraja , na juhudi hizo zimezaa matunda siku ya Jumamosi wakati walipofanikiwa kupata ushindi mwembamba lakini muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Freiburg. Hamburg sasa ina pointi 25 na timu iliyoko juu yake tu ni Freiburg yenye pointi 30.
Hii ina maana timu hizo zinapishana pointi 5 na kumebakia michezo 3 ligi kumalizika. Timu 3 zimefungana katika pointi 30 ambazo ni VFL Wolfsburg, Mainz 05 na Freiburg. Katika michezo mitatu ijayo ya kukunja jamvi la Bundesliga , timu hizo zitakuwa zinaiangalia Hamburg kwa jicho la woga kabla ya kumalizika ligi.
Kama anavyoelezea mshambuliaji wa Hamburg SV Lewis Holtby.
"Wakati huu, lazima niseme , najisikia vizuri sana. Kikosi kizima, nafikiri, kinajisikia vizuri. Ulikuwa ni ushindi mihumu sana leo. Ilikuwa vita, haukuwa mchezo rahisi. Lakini tulitaka kwa vyovyote kupata pointi tatu. Hiyo ilikuwa muhimu. Tulipaswa kuonesha sura yetu ya mapambano. Tuna michezo mitatu sasa, wiki ijayo lijafata mapambano kali ya wababe wa kaskazini. Tunapaswa kucheza kama tulivyocheza na kuonesha kila kitu, ili tuweze kufanikiwa."
Katika nafasi ya kucheza katika ligi ya Ulaya Europa league , TSG Hoffenheim ilisababisha mazungumzo ya kurefusha mkataba wa kocha wa RB Leipzig Ralph Hasenhuttl kusitishwa ghalfa baada ya kisago cha mabao 5-2 nyumbani.
VFB Stuttgart imefanikiwa kubakia katika daraja la kwanza kwa kuifunga Werder Bremen kwa mabao 2-0 kama ilivyokuwa kwa Augsburg ambayo iliishinda Mainz 05 kwa mabao 2-0 pia. Werder Bremen na Hannover 96 bado kimahesabu hazija jihakikishia kubakia katika daraja la kwanza lakini zimo katika nafasi salama zaidi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu