1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokumbwa na maafa ya ufashisti wasema kesi hiyo ni muhimu

21 Aprili 2015

Aliekuwa afisa katika jeshi la mafashisti Oskar Gröning amefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuhusika na maangamizi ya wayahudi na wafungwa wengine kwenye kambi ya Auschwitz wakati wa vita vikuu vya pili.

https://p.dw.com/p/1FBwh
Aliekuwa mlinzi kwenye kambi ya Auschwitz Oskar Gröning
Aliekuwa mlinzi kwenye kambi ya Auschwitz Oskar GröningPicha: DW/B. Knight

Oskar Gröning aliomba radhi kwa kuhusika na mauaji yaliyofanywa kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz iliyojengwa na mafashisti ili kuwaangamiza wayahudi na wafungwa wengine .

Mshtakiwa huyo amesema hakuna shaka kwamba anawajibika kimaadili. Mtu huyo mwenye umri wa miaka 93 anaejulikana zaidi kama mweka mahesabu wa kambi ya Auschwitz alikiri leo mahakamani kwamba alijua juu ya wayahudi walioangamizwa kwa gesi ya sumu katika kambi hiyo na aliomba radhi. Amesema aliona kila kitu. Pia alielezea jinsi mlinzi mmoja wa mafashisti alivyomuua mtoto mchanga kwenye njia ya reli.

Wahalifu wa mwisho kufikishwa mahakamani

Kutokana na umri mkubwa wa watuhumiwa wengi wa uhalifu wa kivita nchini Ujerumani, Gröning anatarajiwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa wa mwisho kufikishwa mahakamani, miaka 70 baada ya wafungwa kukombolewa kwenye kambi za mafashisti.

Mwendesha mashtaka Thomas Will amesema ni muhimu kesi inayomkabili mtu huyo aliekuwa afisa katika jeshi la mafashisti kufikishwa mahakamani .Amesema jambo la kulitilia maanani katika nyakati za sasa ni kuangalia namna "tutakavyoweza kuitatua migogoro."

Makamu wa mwenyekiti wa kamati ya kimataifa ya kambi ya Auschwitz Christoph Hubner amesema kesi hiyo iliyoanzishwa tena ni muhimu kwa sababu wahalifu wengi walikufa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Akabiliwa na mashtaka ya kusaidia katika mauaji

Oskar Gröning anakabiliwa na mashtaka ya kusaidia katika mauaji ya wayahudi waliotokea Hungary waliopelekwa katika vyumba vilivyokuwa vimetiwa gesi ya sumu. Na ikiwa atapatikana na hatia atapewa adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela.

Afisa huyo wa zamani wa jeshi la mafashisti pia alikuwa mwekaji mahesabu aliekusanya na kuzihesabu fedha za wafungwa waliouawa. Pia alichukua vito vya thamani vya wafungwa waliouawa.

Waendesha mashaka wamesema, kwa kufanya kazi kwenye kambi ya mateso, Gröning alihusika na mauaji ya watu zaidi ya Milioni moja, kuanzia mwezi Mei hadi Julai mnamo mwaka wa 1944.

Idadi kubwa ya watu hao walikuwa wayahudi walioangamizwa kabla ya kambi ya Auschwitz kukombolewa na majeshi ya Umoja wa Kisoviet .

Mwandishi:Mtullya Abdu.ZA.afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman