F1: Hamilton ampiku Vettel Ubelgiji
28 Agosti 2017Muaustralia Daniel Ricciardo wa timu ya Red Bull alipanda jukwaani katika nafasi ya tatu. Vettel wa timu ya Ferrari sasa anaangazia macho yake kwa wikendi ijayo, katika mashindano yajayo ya mkondo wa Grand Prix nchini Italia nyumbani kwa kampuni yake ya Ferrari, akiwa kileleni na pengo la pointi saba pekee mbele ya Hamilton. Lakini ana matumaini makubwa "zilikuwa mbio kali sana, kwa sababu kila mzunguko nilikuwa nasubiri Lewis afanye kosa, na hakufanya hivyo. Labda alikuwa anasubiri nifanye kosa na sikufanya kwa hivyo kilikuwa kinyang'anyiro kikali. Nilihofia kuwa sikuwa karibu sana naye, lakini nilikuwa karibu sana sana. Nililazimika kuwa karibu na yakawa mashindano ya kasi kati ya magari mawili na nilikuwa upande wa nje. Sikuwa na mahali pa kwenda"
Hamilton, alifikia rekodi ya Michael Schumacher ya kuanza mashindano 68 akiwa katika nafasi ya kwanza na aliongoza mkondo wa Ubelgiji toka mwanzo hadi mwisho akifuatwa unyounyo na Vettel katika nafasi ya pili. Mercedes wameshinda nne kati ya mashindano matano ya mwisho ya Grand Prix nchini Italia, yakiwemo matatu ya mwisho, lakini Vettel alishinda akiwa na timu ya Red Bull katika mwaka wa 2011 na 2013 na timu ya Toro Rosso katika mwaka wa 2008.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Abdulrahman