1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi inaendelea na mashambulizi yake ya anga nchini Syria

Admin.WagnerD12 Oktoba 2015

Umoja wa Ulaya umeishutumu Urusi kwamba inahatarisha juhudi za amani nchini Syria na kuitaka isitishe kampeni yake ya hujuma za mabomu dhidi ya waasi wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi.

https://p.dw.com/p/1Gmtx
Mawaziri wa mambo ya nje wa Hungary Peter Szijjarto, Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani na Jean Asselborn wa Luxembourg wakizungumza wakati wa mkutano wao mjini Luxembourg.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Hungary Peter Szijjarto, Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani na Jean Asselborn wa Luxembourg wakizungumza wakati wa mkutano wao mjini Luxembourg.Picha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

Hata hivyo mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Luxembourg siku ya Jumatatu, walishindwa kukubaliana kuhusu mchango wa Rais Bashar al-Assad katika kuutanzua mgogoro huo.

Wawaziri hao walionya kwamba mashambulizi ya anga yaliolengwa kumuunga mkono rais Assad yanavitanuwa zaidi vita vya miaka minne na nusu sasa vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na ambavyo vimeshawauwa watu 250,000.

"Mashambulizi ya karibuni ya Urusi ni kitisho kikubwa na lazima yasitishwe mara moja,"walisema mawaziri hao katika taarifa yao iliokuwa na maneno makali.

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherine akiwa mjini Luxembourg kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja huo.
Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherine akiwa mjini Luxembourg kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja huo.Picha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

Hatma ya Assad yawachanganya

Msimamo wa Umoja wa Ulaya wenyewe kuhusu Assad haujulikani wazi, kukiwa hakuna makubaliano iwapo Assad anaweza kutoa mchango katika kupatikana usimamishaji mapigano na kufungua njia ya kufanyika uchaguzi, au ikiwa aende uhamishoni au gerezani.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uhispania Jose Manuel Garcia-Margallo, alisistiza kwamba nchi za magharibi zinapaswa kuzungumza na Assad ili kuituliza hali ya mambo nchini Syria.

"Urusi inasema ikimuacha Assad aondoke madarakani itapoteza ushawishi wake katika eneo hilo na Marekani nayo inasema akiachiwa aendelee nayo itapoteza ushawishi wake kwa tawala za eneo hilo. Kwa hiyo tuna fikra mbili zinazokinzana."

Ama waziri wa masuala ya Ulaya wa Ufaransa Harlem Desir alisistiza kwamba Assad ambaye anachungunguzwa na nchi hiyo kwa uhalifu wa kivita lazima aondoke madarakani mara moja. Kwa upande wake Uingereza imesema Assad hawezi kubakia kuwa rais, lakini itakuwa tayari kuzungumzia suala la vipi na lini ataweza kuondoka madarakani.

Pamoja na hayo taarifa hiyo ilisema kurefushwa kwa mgogoro huo kunahujumu mchakato wa kisiasa, kuhujumu shughuli za usambazaji misaada ya kibinaadamu na kuongeza hisia za itikadi kali.

Kuikosoa kwao Urusi, kumeonekana kupunguwa tangu ulipofanyika mkutano wa Umoja wa mataifa mwishoni mwa mwezi Septemba mjini New York, ambapo Ulaya na marekani ziliitaka Urusi isaidie.

Halikadhalika mipango ya lile kundi la mawasiliano pamoja na Urusi, Marekani Iran na Saudi Arabia kujaribu kutafuta suluhisho la baada ya vita kumalizika nao umefifia, huku maafisa wa kibalozi wa Umoja wa Ulaya wakiwa na fikra chache za jinsi ya kupata suluhisho la kisiasa.

Wanajeshi wa Urusi wakifunga mabomu kwenye ndege kwa ajili ya mashambulizi nchini Syria.
Wanajeshi wa Urusi wakifunga mabomu kwenye ndege kwa ajili ya mashambulizi nchini Syria.Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Kots

Hofu ya kutengeneza Libya nyingine

Mwanadiplomasia mmoja anayehusika na mazungmzo hayo alisema, "wapinzani wakuu wote wa Assad wamekufa wako jela au wanaishi uhamishoni, na hakuna anayetaka patokee Libya nyengine, akidokeza juu ya mfano wa kuporomoka kwa Libya baada ya kuangushwa madarakani Kiongozi wake wa muda mrefu Muammar Gaddafi.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya nao pia wanatarajiwa kuilaani Urusi, watakapokutana kwa mkutano wa kilele Alhamisi ijayo mjini Brussels. Baada ya miaka ya kutochukua hatua madhubuti kuhusu Syria, mataifa hayo 28 ya Umoja wa Ulaya sasa yamo katika kukabiliana na wimbi la wahamiaji wanaokimbilia Ulaya.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/ap

Mhariri:Hamidou Oummilkheir