1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kuilipa Tunisia chini ya mkataba wa kudhibiti uhamiaji

22 Septemba 2023

Umoja wa Ulaya umetangaza leo kwamba utaanza kuipa Tunisia fedha chini ya mpango unaolenga kupunguza idadi ya wahamiaji wanaopitia nchi hiyo kwa kutumia boti kuelekea Italia.

https://p.dw.com/p/4WhjY
Italien | Migranten auf Lampedusa
Picha: Cecilia Fabiano/AP Photo/picture alliance

Umoja wa Ulaya umetangaza kwamba utaanza kuipa Tunisia fedha chini ya mpango unaolenga kupunguza idadi ya wahamiaji wanaopitia nchi hiyo kwa kutumia boti kuelekea Italia.

Msemaji wa Baraza Kuu la Umoja huo Ana Pisonero amesema malipo ya kwanza kiasi cha euro milioni 127 yatatolewa katika siku chache zijazo

"Baraza la Umoja wa Ulaya leo linatangaza bajeti ya euro milioni 60 kama msaada wa bajeti kwa Tunisia na kiasi cha usaidizi wa uhamiaji cha karibu euro milioni 67, ambazo zitatolewa katika siku zijazo, kusainiwa na kuwasilishwa kwa haraka."

Chini ya makubaliano hayo, yaliyosainiwa na rais wa halmashauri kuu ya umoja huo Ursula Von Der Leyen mwezi Julai, Tunisia itapokea milioni 105 kuzuia uhamiaji kinyume cha sheria, milioni 150 katika msaada wa kibajeti na euro milioni 900 ikiwa ni msaada wa muda mrefu.

Tunisia ni kati ya nchi ambako wahamiaji wengi hutokea kwa njia ya boti kuelekea Ulaya kupitia Bahari Mediterania.

Wabunge wa Umoja wa Ulaya pamoja na wanaharakati na mashirika ya misaada kwa wahamiaji yamehoji ikiwa makubaliano hayo na Tunisia yanakidhi viwango vya haki za watu Ulaya.