1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yatangaza hali ya hatari nchi nzima

3 Novemba 2021

Ethiopia imetangaza hali ya hatari iliyoanza kutekelezwa mara kote nchini humo, huku mamlaka ya mji mkuu Addis Ababa ikiwambia raia kujiandaa kuulinda mji huo, wakati wapiganaji kutoka mkoa wa Tigray wakiutishia mji huo.

https://p.dw.com/p/42VX7
Symbolbild Äthiopien Tigray-Krise | Ausnahmezustand
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Shirika la utangazaji linalofungama na serikali la Fana, limesema hali hiyo ya hatari itakayodumu kwa miezi sita, inalenga kuwalinda raia dhidi ya ukatili unaofanywa na magaidi wa kundi la TPLF katika maeneo kadhaa ya nchi.

Miongoni mwa mambo mengine, sheria hiyo ya hali ya hatari inaruhusu kuanzishwa vizuwizi vya barabarani, kuvurugwa kwa huduma za usafiri, kutangazwa marufuku ya kutotembea usiku na kwa jeshi kuchukuwa udhibiti wa baadhi ya maeneo.

Mtu yeyote anaeshukiwa kuwa na mafungamano na "makundi ya kigaidi" anaweza kukamatwa na kuzuwiwa bila waranti wa mahakama, na raia yeyote aliefikia umri wa kutumikia jeshi anaweza kuitwa kupigana. 

Soma zaidi: Wakaazi wa Addis Ababa watakiwa kusajili silaha zao

"Nchi yetu inakabiliwa na hatari kubwa kwa uwepo wake, mamlaka na umoja. Na hatuwezi kuondoa hatari hii kupitia mifumo ya kawaida na taratibu za utekelezaji wa sheria," alisema waziri wa sheria Gideon Timoteos katika mkutano na vyombo vya habari vya serikali.

Karte Äthiopien Region Tigray DE
Waasi wa Tigray wamedai kuuteka mji wa Dessie na sasa wanatishia kusonga mbele hadi mji mkuu Addis Ababa.

Waziri Timoteos alisema yeote atakaekiuka sheria ya hatari atakabiliwa na kifungo cha miaka mitatu hadi kumi, kwa makosa kama vile kutoa msaada wa kifedha, vitu au kimaadili kwa makundi ya kigaidi.

Hatua hiyo imekuja baada ya wapiganaji wa Tigray kusema wameiteka miji ya kimkakati ya Dessie na Kombolcha katika mkoa jirani wa Amhara katika siku za karibuni, na pia wakaashiria huenda wakasonga mbele zaidi kusini kuelekea Addis Ababa.

Serikali imesema wanajeshi walikuwa wanapambana bado kuilinda miji hiyo, iliyoko umbali wa kilomita takribani 400 kutoka mji mkuu.

Sehemu kubwa ya Ethiopia Kaskazini iko chini ya mzingiro wa kimawasiliano na waandishi habari wanadhibitiwa, hali inayofanya madai ya uwanja wa vita kuhakikiwa kwa uhuru zaidi.

Mapema siku ya Jumanne, mamlaka za mji mkuu Addis Ababa ziliwambia wakaazi kuandikishwa silaha zao katika muda wa siku mbili zijazo na kujiandaa kuulinda mji huo.

Biden aitoa Ethiopa kwenye AGOA

Mjini Washington, rais Joe Biden ametangaza kuiondoa Ethiopia kutoka mpango wa biashara unaojulikana kama Sheria ya Ukuaji na Fursa, AGOA, kutokana na ukiukaji wa haki zinazotambulika kimataifa za binadamu.

Soma zaidi: Shinikizo laongezeka dhidi ya serikali ya Ethiopia kuhusu jimbo la Tigray

Biden ameliambia bunge la Marekani kwamba ustahiki wa Ethiopia katika mpango huo utamalizika Januari Mosi mwakani.

Mpango wa kihistoria wa AGOA uliopitishwa mwaka 2000, unatoa fursa kwa mataifa ya Afrika kusini mwa Sahara, kuuza bidhaa zao nchini Marekani bila kutozwa ushuru, kwa sharti la kuzingatia utawala bora.

Äthiopien | Mekele | Verwundete äthiopische Gefangene im Mekele Rehabilitation Center
Wanajeshi wa Ethiopia waliotekwa na wapiganaji wa Tigray wakiwa wamekusanywa baada ya kuoneshwa mitaani katika mji wa Makele, Tigray, Oktoba 22, 2021.Picha: AP Photo/picture alliance

Ethiopia ambayo katika wiki za karibuni ilifanya uraghibishi kusalia katika mpango wa AGO, imesema imevunjwa moyo na uamuzi huo.

"Matendo hayo yatapindua mafanikio makubwa ya kiuchumi katika nchi yetu na kuathiri isivyo haki na kuwaumiza wanawake na watoto," alisema taarifa ya wizara ya biashara.

Mauzo ya Ethiopia nchini Marekani yamepanda kutoka dola milioni 28 mwaka 2000 hadi karibu dola milioni 300 mwaka 2020, huku karibu nusu ya bidhaa zikiangukia chini ya AGOA, kwa mujibu wa serikali ya Abiy.

Baadae siku ya Jumanne, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilitoa tadhari mpya kwa ajili ya Ethiopia, na kusema raia wa Marekani "wanapaswa kuzingiatia kuondoka sasa" kwa kutumia ndege za kibiashara.

Chanzo: Mashirika.