Ethiopia kuchunguza mauaji ya raia mpaka wa Saudia-Yemen
23 Agosti 2023Serikali ya Ethiopia imesema itaichunguza ripoti ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch ya mauaji ya mamia ya raia wake kwenye mpaka wa Yemen na Saudi Arabia.
Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ethiopia imesema uchunguzi huo utafanywa kwa ushirikiano na maafisa wa Saudia.
Human Rights Watch yenye makao yake mjini New York ilitoa ripoti Jumatatu ikitaja simulizi za mashuhuda wa mashambulizi yaliyofanywa na walinzi wa mpakani nchini Saudi Arabia wakitumia bunduki za rashasha na maguruneti dhidi ya Waethiopia ambao hawakuwa na silaha waliojaribu kuingia katika taifa hilo la Kifalme kutokea Yemen.
Wizara hiyo imetoa wito wa kujizuia na kushauri dhidi ya kusambaza uvumi wowote hadi pale uchunguzi utakapokamilika, ikiongeza kuwa nchi hizo mbili zina mahusiano mazuri ya muda mrefu. Afisa mmoja wa Saudia amesema ripoti ya HRW haikuwa na msingi wowote na haikuzingatia vyanzo vya kuaminika, lakini hakutoa ushahidi wowote wa kuthibitisha madai hayo.