Eritrea yaongoza orodha ya nchi 10 zinazobana habari huru
10 Septemba 2019Nchi tatu zinaongoza orodha hiyo -Eritrea, Korea ya Kaskazini na Turkmenistan- na katika nchi hizo vyombo vya habari "vinatumiwa kama chombo cha kuipigia upatu serikali na vyombo vyote huru vya habari vinaendesha shughuli zake kutoka uhamishoni-" limesema shirika hilo lenye makao yake nchini Marekani na ambalo limepania kuhakikisha waandishi habari wanalindwa-CPJ.
Mataifa mengine katika orodha hiyo ya mataifa 10 ambako vyombo vya habari vinakandamizwa na serikali " yanatumia mchanganyiko wa mbinu mfano vitisho na kukamata watu ovyo ovyo sawa na kuwapeleleza na kujaribu kuvinyamazisha vyombo huru vya habari.
Saudi Arabia, China, Vietnam na Iran zimetajwa kwa kuwafunga na kuwasumbua waandishi habari na familia zao huku zikifanya kila la kufanya kuvipeleleza vyombo huru vya habari kwa njia za digitali, kufunga mawasiliano kwa njia ya intaneti na mitandao ya kijamii.
Mpangilio wa orodha hiyo umefuata vipengele ambavyo ni pamoja na vizuwizi vya kumiliki au kuwepo vyombo huru vya habari, sheria za uhalifu zinazomchafulia mtu hadhi yake, tovuti kufungwa, waandishi habari kuchunguzwa na maafisa wa serikali, masharti ya kutolewa vibali kwa vyombo vya habari, udukuzi na kadhalika.
Mtandao wa Interneti haukufanikiwa kulifikia lengo lake
Mtandao wa intaneti ulilengwa kuufanya mtindo wa kuvikagua vyombo vya habari upitwe na wakati, lakini shabaha hiyo haikuweza kufikiwa" amesema mkurugenzi mkuu wa shirika linalopigania kulindwa waandishi habari CPJ, Joel Simon.
"Nchi nyingi zinazodhiti vyombo vya habari zinadhibiti pia mawasiliano ya kimamboleo na zinaendesha harakati zake kupitia mitandao ya intaneti. Serikali za nchi hizo zinachanganya mitindo ya zamani ya kikatili na teknolojia ya kimamboleo ambayo mara nyingi huuzwa na makampuni ya nchi za magharibi, amesema Joel Simon.
Ripoti ya shirika la CPj inajumlisha nchi kumi ambako serikali zinadhibiti vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na Guinea ya Ikweta, Belorusia na Cuba.
Ripoti hiyo imeongeza kusema katika nchi nyengine ikiwa ni pamoja na zile zilizoteketezwa kwa vita mfano wa Syria, Yemen na Somalia vyombo vya habari vinakabiliwa na shida kubwa ingawa sio lazima shida hizo ziwe zinasababishwa pekee na serikali.
Nchini Eritrea, serikali ndio inayodhibiti mamlaka ya vyombo vya habari na vyanzo mbadala vya habari mfano intaneti, au matangazo kupitia satelaiti na vituo vya matangazo kutoka uhamishoni vinazuiliwa na kuchunguzwa na idara maalum za serikali.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Josephat Charo