Erdogan: Mkataba wa nafaka kufufuliwa karibuni
5 Septemba 2023Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema itawezekana katika siku chache zijazo kuufufua mkataba wa nafaka ambao Umoja wa Mataifa unasema ulisaidia kupunguza mgogoro wa chakula kwa kufikisha nafaka ya Ukraine katika soko la dunia. Erdogan ameyasema hayo baada ya kukutana ana kwa na kwa mara ya kwanza tangu 2022 na rais wa Urusi Vladimir Putin katika mji wa mapumziko wa Sochi katika bahari Nyeusi.
Putin alisema mkataba huo hautafufuliwa mpaka nchi za Magharibi zitakapotimiza masharti ya Urusi kuhusu mauzo ya nje ya bidhaa zake za kilimo. Erdogan amesema matarajio ya Urusi yanafahamika na wote na kwamba mapungufu yanatakiwa yatatuliwe. Pia amesema Uturuki na Umoja wa Mataifa wameandaa mapendekezo kadhaa mapya kupunguza wasiwasi wa Urusi.
Erdogan ameitaka Ukraine ilegeze msimamo wake dhidi ya Urusi katika mazungumzo kuhusu kuufufua mkataba wa nafaka na isafirishe nafaka zaidi barani Afrika badala ya Ulaya.