Erdogan awataja wagombea wa chama katika uchaguzi wa Machi
7 Januari 2024Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amewataja wagombea kadhaa wa chama chake watakaowania nafasi katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Machi. Chama tawala kitajaribu kujiimarisha na kuitwaa miji iliyochukuliwa na chama cha upinzani cha Republican People, CHP, miaka mitano iliyopita, ukiwemo mji mkubwa kabisa wa Uturuki, Istanbul, na mji mkuu, Ankara.
Erdogan amesema mbunge na waziri wa zamani wa mazingira na ukuaji wa miji, Murat Kurum, atapambana na Ekrem Imamoglu, meya wa upinzani wa mji wa Istanbul, ambaye ametambuliwa kitaifa. Wengi walitarajia Imamoglu kushindana na Erdogan katika uchaguzi wa rais mwaka uliopita. Erdogan ameuambia mkutano mkuu wa chama tawala, Justice and Development - AKP - mjini Istanbul kwamba mji huo utafanikiwa kutimiza azma yake na hauwezi kupoteza kwa miaka mingine mitano.