Erdogan atangaza sheria ya hali ya hatari kwa miezi mitatu
21 Julai 2016Hayo yamefuatiwa na kukamatwa na majaji wengine 32 na maafisa wawili wa jeshi wakihusishwa na njama hizo, huku Ujerumani ikipaza sauti yake dhidi ya kile kinachoonekana kama kuyatumia mapinduzi kuukandamiza wa upinzani kwa mshirika wake huyo muhimu.
Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni usiku wa jana, Rais Erdogan alisema uamuzi wa kutangaza hali ya hatari ni kupambana na kile alichokiita ugaidi.
"Lengo la tangazo hili la hali ya hatari ni kuweza kuchukuwa hatua muafaka ili kuondosha kabisa kitisho cha magaidi haraka iwezekanavyo, ambacho ni kitisho kwa demokrasia, utawala wa sheria na haki na uhuru wa raia wa nchi yetu. Hili halihusiani kabisa na kuiandama demokrasia, bali kuimarisha na kulinda maadili yetu." Alisema Erdogan.
Bunge linakutana leo kuliidhinisha rasmi tangazo hilo. Afisa mmoja wa serikali ameliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa, kuwa hali hiyo ya hatari inalenga kuwashughulikia wafuasi wa hasimu mkubwa wa Rais Erdogan, Fethullah Gulen, anayeshutumiwa kuwa kiongozi wa njama hiyo ya mapinduzi.
Kwa mujibu wa afisa huyo aliyekataa kutajwa jina, hali hiyo ya hatari itatumika kupambana na "mfumo mbadala", neno linalotumiwa na serikali kumkusudia Gulen, kiongozi wa kidini anayeishi uhamishoni nchini Marekani.
Gulen asema haogopi kurudi Uturuki
Tayari serikali ya Uturuki inasema imeiomba Marekani kumrejesha Gulen ili akabiliane na kesi ya uhaini, lakini msemaji wake, Alp Aslandogan, anasema Gulen hana wasiwasi wowote.
"Hatuna wasiwasi wowote. Bwana Erdogan aliwahi kuzungumzia haya ya kumtaka Gulen arejeshwe miaka miwili iliyopita na kila mara amekuwa akiyasema ingawa hadi sasa hawajatuma maombi rasmi. Japo kuna habari kuwa wametuma, lakini ukweli ni kuwa walichotuma hakitambuliwi kama ombi rasmi. Yumkini kitatambuliwa baadaye, lakini ikiwa taratibu zitafuatwa sisi hatujali."
Haya yanajiri wakati kamatakamata na fukuzafukuza ikiendelea nchini Uturuki. Kufikia asubuhi ya leo, watu 10,000 walikuwa wameshawekwa kizuizini, huku vyuo na skuli kadhaa zikifungwa, na wahadhiri na wakuu wa vitengo vyuoni humo wakiwekwa ndani. Takribani wafanyakazi 60,000 wa sekta ya umma wamefutwa kazi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, ameitolea wito Uturuki kutekeleza hatua hizo za hali ya hatari kwa kipindi maalum tu, na kuzikomesha haraka iwezekanavyo.
Steinmeier, ambaye nchi yake inakaliwa na jamii kubwa ya Kituruki, amesema si sahihi hali hiyo kutumiwa kwa malengo ya kuwaandama wanasiasa, ambao hawahusiki kabisa na jaribio hilo la mapinduzi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga