Elimu ya jamii
19 Oktoba 2010Vijana wengi barani Afrika hutafuta maisha kwa mapana na marefu katika enzi hii ya utandawazi, na kisha miongoni mwa jamii iliyoelimika. Hivyo mara nyingi hujikuta katika hali ya kuchanganyikiwa kuhusu njia wanayoweza kuifuata kufikia ufanisi wa taaluma zao. Vipindi vya Noa Bongo vinakuwezesha kufahamu jinsi ulimwengu sasa ulivyo na miujiza ambayo wengi wetu hatuifahamu.
Elimu na vyombo vipya vya habari
Katika mfululizo wa vipindi vya Noa Bongo kuhusu elimu ya chuo kikuu, tuliweza kufuatilia maisha ya msichana mmoja anayetoka kijijini na kujiunga na chuo kikuu jijini kusomea digrii katika masuala ya kilimo. Uliweza kufuatilia hadithi yake anapojaribu kujifahamisha na kuzoea maisha ya jiji na shughuli zake za masomo chuoni.
Vipindi hivi vya Noa Bongo pia vilikufungulia pazia kuhusu masuala ya kompyuta na huduma za Intaneti. Na katika ripoti zetu maalum na vipindi vya redio tuliweza kujifunza mengi kuhusu teknolojia ya mawasiliano ya kisasa - kuanzia mkahawa unaotoa huduma bora hadi kuunganishwa na marafiki kupitia mtandaoni kote duniani.