Ebola yawasili Mali na New York
24 Oktoba 2014Daktari huyo ambaye vyombo vya habari vimelitambua jina lake ni Craig Spencer mwenye umri wa miaka 33 amelazwa katika wodi ya wagonjwa waliotengwa katika hospitali ya Bellevue baada ya kuugua.
Hicho ndicho kisa cha kwanza kuripotiwa katika mji wa New York ulio na wakaazi wengi lakini meya wa mji huo Bill de Blassio amesema hakuna sababu kwa wakaazi wa mji huo kuingiwa na hofu.
Spencer ambaye alikuwa akiwatibu wagonjwa wa Ebola nchini Guinea akiwa chini ya shirika la madaktari wasio na mipaka MSF aliwasili mjini New York Ijumaa iliyopita na hakuonyesha dalili za ugonjwa huo hadi jana asubuhi.
Waliokutana kwa karibu na mgonjwa kuchunguzwa
Watu watatu waliokutana naye kwa karibu, marafiki zake wawili na mchumba wake watachunguzwa kwa siku ishirini na moja zijazo kama wataonyesha dalili za ugonjwa huo. Shirika la kudhibiti magonjwa la Marekani CDC limesema Spencer alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu katika uwanja wa ndege wa JFK lakini hakupatikana na dalili za Ebola.
Mali pia imethibitisha kisa cha kwanza cha Ebola hapo jana, na hivyo kuifanya nchi ya sita ya magharibi mwa Afrika kurekodi Ebola. Waziri wa afya wa Mali Ousmanne Kone amesema msichana wa umri wa miaka miwili aligunduliwa na virusi vya Ebola.
Msichana huyo aliwasili mjini Bamako siku kumi zilizopita kutoka Guinea akiwa ameandamana na jamaa zake na baadaye kuelekea katika mji wa magharibi mwa Mali wa Kayes ambako alipelekwa hospitalini siku ya Jumatano baada ya kuugua.
Kone amesema hali ya msichana huyo inaimarika baada ya kupokea matibabu ya haraka na kuongeza jamaa zake wameshatambuliwa na maafisa wanachukua kila hatua kuhakikisha ugonjwa huo hausambai.
Nchi za Afrika kutuma wahudumu wa afya
Hayo yanakuja wakati ambapo Umoja wa Afrika umetangaza nchi wanachama zimeahidi kutuma wahudumu wa afya takriban 1,000 nchini Guinea, Liberia na Sierra Leone, nchi zilizoathirika zaidi na Ebola ili kujaribu kuudhibiti ugonjwa huo.
Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imeahidi kutuma wahudumu 1,000 wa afya, nchi za Afrika Mashariki zilikuwa zimeahidi kuwapeleka wahudumu 600 na Nigeria imeahidi itatuma kundi la wahudumu 600 katika nchi hizo.
Na Umoja wa Ulaya umesema unapania kuchangisha euro bilioni moja kusaidia katika juhudi za kupambana na Ebola. Hapo jana umoja huo ulitangaza msaada wa euro milioni 24.4 kusadia katika utafiti wa kupatikana kwa chanjo na tiba.
Rais wa halmashauri ya umoja huo Jose Manuel Barrosso ameelezea matumaini kuwa anataraji nchi za umoja huo zitaahidi misaada zaidi hii leo katika mkutano wa kilele wa viongozi wa umoja huo unaofanyika mjini Brussels.
Shirika la afya duniani WHO ambalo lilifanya mkutano wa dharura hapo jana kujadili janga la Ebola limesema ugonjwa huo ambao umewaua kiasi ya watu 4,900 unasalia kutia wasiwasi mkubwa huku visa vikiongezeka kwa kiwango kisichoweza kutabirika.
Mwandishi:Caro Robi/Reuters/ap/dpa
Mhariri:Josephat Charo