1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola: Hali nchini Liberia ni ya kutisha

10 Septemba 2014

Waziri wa ulinzi wa Liberia ameonya kuwa Ebola inatishia kuwepo kwa taifa hilo wakati virusi hivyo hatari vikisambaa kama “moto wa kichakani”. Nalo Shirika la Afya Ulimwenguni limesema idadi ya vifo inaongezeka

https://p.dw.com/p/1D9e5
Ebola in Liberia 09.09.2014
Picha: picture-alliance/dpa/A. Jallanzo

Baada ya kutabiri kuwa maambukizi ya ugonjwa huyo yatafikia kiwango cha juu kote Afrika Magharibi, Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO, limeonya kuwa Liberia ambayo imeshuhudia nusu ya jumla ya idadi ya vifo vilivyoripotiwa huenda kwanza ikatarajia tu kupunguza usambaaji wa virusi hivyo, na wala siyo kuzuia.

Waziri wa ulinzi wa Liberia Brownie Samukai ameuambua mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa “Liberia sasa inakabiliwa na kitisho kikubwa cha kuwepo kwake kama taifa”. Amesema ugonjwa huo unasambaa kwa kasi kama “moto wa kichakani, huku ukikiteketeza kila kitu njiani mwake”

Sierra Leone Ebola
Karin Landgren mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia anasema hali itaendelea kuwa mbayaPicha: picture-alliance/dpa/N. Shrestha

WHO imesema idadi ya vifo vya Ebola imeongezeka hadi kufikia 2,296 kati ya visa vya maambukizi 4,293 nchini Liberia, Sierra Leone, Guinea na Nigeria kufikia Septemba 6. Takribani nusu ya maambukizi yote yalitokea katika kipindi cha siku 21 zilizopita. Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia, Karen Landgren anasema ugonjwa huo unasambaa nchini humo ''Bila huruma''.

Shirika hilo pia limemhamisha mtalaamu wake wa pili wa matibabu aliyeambukuzwa wakati akifanya kazi katika kituo kimoja cha matibabu ya Ebola nchini Sierra Leone. Takwimu za hivi karibuni za WHO zinadhihirisha usambaaji wa kiholela wa Ebola, wakati ugonjwa huo ukijipenyeza katika jamii zilizojaa watu bila vifaa maalum vya matibabu na zinazokosa kampeni za uhamasisho wa umma kuhusiana na mlipuko huo.

Mkuu wa kitengo cha magonjwa wa WHO Sylvie Briand anasema lengo la sasa nchini Senegal na Nigeria ni “kuzuia kabisa maambukizi ya ugonjwa huo”. SENEGAL imetangaza kisa kimoja pekee cha maambukizi wakati Nigeria ikiorodhesha visa 19 vya maambukizi na vifo vya watu wanane. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inapambana kuukabili mlipuko mwingine uliowauwa watu 32 katika eneo moja la kaskazini magharibi.

Karin Landgren
Kumekuwa na migomo ya wauguzi nchini Sierra Leone na Liberia kuhusiana na mazingira ya kaziPicha: DOMINIQUE FAGET/AFP/Getty Images

Briand amesema mjini Geneva kuwa “katika maeneo mengine kama Monrovia, ambako kuna kiwango kikubwa cha maambukizi, wanalenga kutumia mikakati ya hatua mbili. Kwanza ni kupunguza maambukizi kadri inavyowezekana, na wakati hali hiyo itakapodhibitiwa, watajaribu kuumaliza ugonjwa huo kabisa.”

Rais wa Guinea Alpha Conde ameutaja ugonjwa wa Ebola huo kuwa ni “vita nchini mwake – huku kukiwa na vifo vya watu 555 kufikia sasa”. Amezishutumu nchi jirani ikiwa ni pamoja na Cote d'Ivoire na Senegal kwa kufunga mipaka yao na mashirika ya ndege kusitisha safari zao katika nchi zilizoathirika. Siku ya Jumatatu Umoja wa Afrika ulitoa wito wa kufunguliwa mipaka ya nchi hizo na pia marufuku ya safari za ndege kuondolewa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel