Ebola bado yaenea Sierra Leone na Guinea
10 Desemba 2014Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva jana jioni, David Nabarro amesema maeneo hayo ya Guinea na Sierra Leone ambayo bado yanatishiwa na kitisho cha Ebola yanahitaji wataalamu wa tiba kutoka nje, madawa, vifaa na vitanda zaidi. Amesema litakuwa kosa kubwa kujidanganya kwamba mapambano dhidi ya Ebola yamefanikiwa kwa kiwango chochote, wakati yakiwepo maeneo ambayo bado yanao ugonjwa huo, kwani yaweza kuwa rahisi kwa maambukizi hayo kuanza kusambaa tena.
Nabarro alisema, ''Hatuwezi kujiridhisha na kusema kazi imekamilika, hata kwa kiwango chochote, kwa sababu ya wasiwasi ambao umekuwepo muda wote kwamba ikiwa yapo maambukizi sehemu yoyote, yanaweza kusambaa tena hadi kufika maeneo mapya. Kwa sababu hiyo yatubidi kuendelea kuwa makini, na kuamka kila siku tukijua bado tunayo kazi kubwa ya kufanya.''
Lakini, mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola alisifu kazi inayofanywa katika maeneo mengine ya Afrika magharibi, katika kusimamisha maambukizi mapya ya Ebola. Taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Afya Ulimwenguni imeonyesha kuwa kwa wakati huu kiwango cha maambukizi ya Ebola ni kikubwa nchini Sierra Leone kuliko kile cha nchini Guinea.
Ripoti kutoka nchini Sierra Leone zimeeleza kuwa madaktari wameendelea na mgomo waliouanza Jumatatu, ambao wanauita ''mkakati wa kurudi nyuma'' unaolenga kuyapa msukumo madai yao ya kutaka huduma bora kwa wauguzi wanaoambukizwa ugonjwa wa Ebola wakiwa kazini, hiyo ikifuatia vifo vya wafanyakazi wengi katika sekta ya afya kutokana na ugonjwa huo.
Tangu mlipuko wa sasa wa Ebola kutokea, mamia ya wahudumu wa afya wameambukizwa ugonjwa huo, lakini hali imeripotiwa kuwa mbaya zaidi nchini Sierra Leone. Ripoti ya Kituo cha Marekani kinachoshughulia magonjwa ya kuambukiza CDC, ilisema kiwango cha maambukizi miongoni mwa wafanyakazi wa afya nchini Sierra Leone ni kikubwa mara 100 ikilinganishwa na watu wazima wengine wanaofanya kazi katika sekta nyingine.
Kampeni ya kutokomeza Ebola yazinduliwa
Wakati huo huo rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf alianzisha kampeni iliyoitwa ''Lazima Ebola Itokomezwe'', ambamo amewataka wakazi wa nchi yake kutolegeza kamba hata kidogo katika kujilinda maambukizi ya ugonjwa huo.
Katika hotuba yake rais Sirleaf amesema juhudi za kupambana na Ebola zimefanikiwa katika maeneo mengi ya nchi, na kutaka njia muafaka zitafutwe kuufuata katika maeneo ambako bado unatishia maisha. ''Kutokana na juhudi zetu, Ebola imerudishwa nyuma hadi maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa. Kwa sasa uko katika jamii za vijiji vya mbali, ambako lazima tutafute njia ya kufika. Sote kwa pamoja tunapaswa kusema kwa dhati lazima Ebola ishindwe.''
Liberia imeandaa mazungumzo baina ya nchi zilizoathiriwa zaidi na Ebola pamoja na ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu ugonjwa huo, katika juhudi za kuweka mkakati wa pamoja kuzuia maambukizi yanayovuka mipaka ya mataifa.
Mwandishi:Daniel Gakuba/ape/afpe
Mhariri:Josephat Charo