DW yazindua makala mpya za "Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani"
19 Desemba 2023DW imezindua mradi wake mpya wa mfululizo wa makala kuhusu historia ya Ujerumani ambazo zinaangazia sifa ya ukoloni wa Ujerumani barani Afrika. Kupitia mtazamo wa Kiafrika, vipindi kumi vinaelezea jinsi Ujerumani ilivyokuja kujiunga baadaye katika kinyang'anyiro hicho, ilivyokumbana na upinzani mkali, na ilivyojihusisha na unyanyasaji na ukatili. Vidio na vipindi hivi vya redio pia vinaangalia jinsi ukoloni wa Ujerumani unavyoendelea kuwepo katika maisha ya sasa.
Hafla ya kufana ya uzinduzi wa mradi huu mpya ilifanyika jijini Dar es Salaam Desemba 14, 2023 na kuhudhuriwa na wadau mbali mbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu na watalaamu wa historia.
Watalaamu wa historia waliohudhuria uzinduzi huo walidokeza kuwa mtizamo wa pamoja kuhusu historia ya ukoloni unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Ujerumani.
Akizungumza katika jopo lililojadili hali ya uhusiano wa baada ya ukoloni kati ya Tanzania na Ujerumani, Mhadhiri wa chuo cha DUCE Dr. Yovita Vakolavene alisema vivuli vya ukatili uliofanywa na Wajerumani bado vinaendelea kuwepo katika maisha ya kila siku ya Waafrika. Katika mjadala huo, masuala ya fidia, kuomba radhi, na ushirikiano yalijitokeza. Washiriki walisema ushirikiano wa nchi hizo mbili utategemea na namna Ujerumani itaendeleza juhudi za kuyatambua yaliyotokea nyuma, kama alivyofanya Rais Frank-Walter Steinmeier wakati alipozuru nchini Tanzania. Dr. Vakolavene aliutolea mfano wa vita vya Maji Maji, ambavyo viliacha alama kubwa katika jamii za Tanzania, akipendekeza kuwa Ujerumani inapaswa kuzisaidia jamii zilizoathirika kwa kuwafanyia miradi mbalimbali ya maendeleo, kama njia moja ya kuyaponya makovu.
Kizazi cha sasa hakina hamasa ya kufahamu historia ya ukoloni
Bi. Vakolavene alikiri kuwa kizazi cha sasa cha Tanzania hakina hamasa ya kufahamu historia ya ukoloni wa Ujerumani, akiongeza kuwa mradi huu wa DW utasaidia kuwapa vijana nafasi ya kusoma zaidi. "Tubadilishe mfumo, watoto waanze kuwa na bidii ya kusoma vitabu na pia kupitia majukwaa ya kidijitali, kuanzia shule za msingi, ili wanapofika elimu ya juu wanakuwa na uelewa mpana sana na kuyachambua mambo kwa upana zaidi". Alisema Dr. Vakolavene.
Vipindi hivi kumi vinaonesha wahusika muhimu wa Kijerumani na Kiafrika kupitia mradi ambao ni ushirikiano wa DW, kampuni ya kuchora vibonzo ya Nigeria – The Comic Republic – na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ambayo imeufadhili mradi huu. Mfululizo wa vipindi hivyo unaangazia mada mbalimbali za ukoloni wa Ujerumani barani Afrika na kuufanya ueleweke zaidi.
Kwa pamoja, hadithi hizo fupi zinatengeneza picha pana ya mzigo mkubwa wa aibu iliyoachwa na utawala wa Wajerumani. Himaya ya Ujerumani ilinyakua ardhi ambazo leo ni za nchi kama vile Togo na Ghana ("Togoland”), Cameroon na Nigeria ("Kamerun”), Namibia ("Afrika Kusini Magharibi ya Wajerumani”), Rwanda, Burundi na Tanzania (Afrika Mashariki ya Wajerumani). Utawala wa Wajerumani katika maeneo hayo ulidumu kuanzia mwaka wa 1884 hadi 1918.
Jamii bado zina uchungu kutokana na ukatili wa kihistoria
Cece Mlay, mtengezafilamu aliyekuwa mmoja wa walioshiriki mjadala huo wa Dar es Salaam, alipongeza hatua ya serikali ya Ujerumani kuyatambua maovu yaliyofanywa katika enzi ya ukoloni, lakini akasisitiza kuwa jamii zilizoathirika zinapaswa kusaidiwa kujijenga, akitolea mfano jamii ya Wachagga ambayo bado inasubiri fuvu la aliyekuwa kiongozi wao Mangi Meli, na Wahehe ambao wanadai fuvu la Chifu Mkwawa. "Kuna familia ambazo mpaka sasa zinaendelea kuumia, zina uchungu, mabaki ya wapendwa wao bado yako Ulaya. Ni muhimu juhudi ziongezwe ili kurejeshwa nyumbani mabaki ya wapigania uhuru hao, ili familia zao zipate amani moyoni."
"Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani" ni mradi uliojengwa juu ya masuala ambayo DW iliyaona mwaka uliotangulia wakati wa kutengeneza toleo la "Mizizi ya Afrika”. Toleo hili jipya litasambazwa katika lugha sita (Kiswahili, Kihausa, Kiamhara, Kiingereza, Kifaransa na Kireno) katika matangazo ya DW na mitandao ya kijamii na kupitia karibu washirika 300 wa vyombo vya habari barani Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa Idhaa za Kiafrika za DW, Bwana Claus Stäcker, anasisitiza kuwa historia ya ukoloni inaathiri mahusiano kati ya Afrika na Ujerumani hadi hii leo: "Tuna mipaka ambayo ilichorwa kwenye ubao zama hizo, ambayo bado inaendelea kuwepo. Vipo vifaa vilivyoporwa na hata mabaki ya miili ya wapigania uhuru ambayo yamehifadhiwa katika makumbusho za Ujerumani.” Kwa miongo mingi mada hizi zilijadiliwa tu miongoni mwa watalaamu, anaongeza Stäcker ambaye anachukizwa na ukosefu wa ufahamu, kwa upande wa Afrika na pia kwa upande wa Ujerumani: "Kupitia Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani, DW inatoa fursa ya kuelimisha – kwa ajili ya siku zijazo. Vidio zilizotengenezwa zinakilenga kizazi cha simu za kisasa za mkononi kwa maana ya mtindo na usimuliaji wa hadithi.”