DW inakuletea mchezo kuhusu Elimu ya Kidijitali Afrika
Katika mji wa Inzuna, barani Afrika, binamu watatu wanaishi kwenye nyumba moja na wanakumbana na tukio lisilotarajiwa katika ulimwengu wa kidijitali.
Mwizi wa taarifa za watu
Aloyce Michael (Kushoto) aliyeigiza kama Rahim, Mzome Mahmud (katikati) aliyeigiza kama Agong, na Rachel Kubo (Kulia) aliyeigiza kama Jennifer, wakiigiza sehemu ambayo Angong alidukua akaunti za mitandao ya kijamii za Jennifer. Pia alijaribu kumlaghai Rahim, lakini hakujua kama atakutana na gwiji wa teknolojia. Agong pia aliwahi kuwa mpenzi wa Jennifer.
Mashambulizi ya mtandaoni yanaongezeka
Mzome Mahmud (kushoto) aliyeigiza kama Agong, Rachel Kubo (katikati) aliyeigiza kama Jennifer, na Happiness Stanslaus (kulia) aliyeigiza kama Faith. Agong anahusika na mashambulizi ya mtandaoni, na pia mlaghai huyu anadukua akaunti ya benki ya Faith.
Juhudi za kupambana na uhalifu wa mtandaoni
Maafisa wa polisi Hassan Kazoa, (kushoto) na Mohammed Kaboba (katikati) waliokuwa wakiwahoji Jennifer na Faith baada ya Rahim kuvamiwa na Agong, wanachukua alama za vidole kwenye dirisha la chumba cha kulala cha Rahim.
Kazi inaendelea
Fundi mitambo, Michael Springer na Grace Kabogo, mtayarishaji, mratibu na muongozaji mkuu wa vipindi vya Noa Bongo-Jenga Maisha Yako, wakiendelea na majukumu yao wakati wa kurekodi mchezo wa Elimu ya kidijitali. Kabla ya kurekodi, huwa wanajadiliana kuhusu mchakato mzima utakavyofanyika.
Usidharau ushauri wa mtaalamu wa teknolojia
Tumaini Mwambasi aliyeigiza kama Nina na Salum Mgoli aliyeigiza kama Paul, msimamizi wa jengo la shule wanayofundisha Nina na Faith. Nina ni mwalimu mwenzake Faith. Kwenye mchezo wa Kisasi cha Mlaghai, Paul anagundua kuhusu ulaghai uliofanywa na mdukuzi, na mashambulizi ya kimtandao dhidi ya Nina na Faith.
Furaha ya waigizaji wakuu studio
Happiness Stanslaus (kushoto) aliyeigiza kama Faith, Rachel Kubo (kulia) aliyeigiza kama Jennifer, na Aloyce Michael (aliyesimama) aliyeigiza kama Rahim, wakiwa na Grace Kabogo, (katikati) mtayarishaji, mratibu na muongozaji mkuu wa vipindi vya Noa Bongo-Jenga Maisha Yako. Binamu hawa wamepambana na fitna za kidijitali na uaminifu wa familia.
Wakati wa kujiandaa
Kati ya kila tukio, huwa kuna muda wa kupumzika na kupitia hadithi zinazofuata. Pichani ni Rachel Kubo aliyeigiza kama Jennifer, na Alocye Michael aliyeigiza kama Rahim, wakijiandaa kabla ya kurekodi sehemu inayofuata ya mchezo.
Mgeni karibu studio
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Daniel Gakuba (mwenye shati la drafti) alipotembelea studio za Lbe, Dar es Salaam, Tanzania kujionea jinsi kazi inavyoendelea. Hapa akiwa na timu ya LbE Kiswahili na baadhi ya waigizaji.
Ushindi wa kazi
Timu ya LbE Kiswahili: Fundi mitambo, Michael Springer (Kulia), Grace Kabogo, (katikati) mtayarishaji, mratibu na muongozaji mkuu wa vipindi vya Noa Bongo-Jenga Maisha Yako na Simon John (kushoto) mtayarishaji msaidizi, waliofanikisha kurekodiwa mchezo mpya wa ''Elimu ya Kidijitali'', hadithi inayoangazia changamoto zinazowakabili vijana wa Kiafrika katika ulimwengu wa kidijitali.
Jennifer, mtu mwenye ushawishi mitandaoni, Rahim, gwiji wa teknolojia, na Faith, mwalimu anayeipenda kazi yake, wanaunda timu isiyotarajiwa wanaposaidiana kupambana na majaribu ya kidijitali. Safari yao inawakutanisha na wadukuzi, walaghai na changamoto zinazowakabili katika ujuzi wao wa kidijitali.