Dunia yakumbuka miaka 75 kukombolewa kambi ya Auschwitz
27 Januari 2020Wazee wa Kiyahudi kutoka Israel, Marekani, Australia, Peru, Urusi na Slovania, wengi wao wakiwa wale waliopoteza wazazi na ndugu kwenye kambi hiyo na nyenginezo zilizoendeshwa na Wanazi, wanasindikizwa leo na watoto na wajukuu na hata vitukuu vyao kwenye kambi ya mauti ya Auschwitz-Birkenau, eneo ambalo miaka 75 iliyopita lilikuwa alama ya dhuluma kubwa dhidi ya binaadamu ilitendwa.
Hata hivyo, mkuu wa jumba la makumbusho la Auschwitz, Piotr Cywinski, ameonya juu ya kile alichokiita kimya cha ulimwengu dhidi ya yanayojiri sasa. "Miaka miwili tu iliyopita, dunia ilishuhudia mauaji ya maangamizi dhidi ya jamii ya Rohingya nchini Myamnar, lakini hakuna aliyejali," alisema mkuu huyo wa makumbusho ya Auschwitz, akiongeza kuwa dunia pia inanyamazia kimya "yanayofanywa na serikali ya China dhidi ya Waislamu wa jamii ya Uighur."
Siku ya Jumapili (Januari 26), Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine alizungumza na manusura wa mauaji hayo ya maangamizi, akiwaita kuwa mashujaa waliosalia kuelezea kipimo cha ubinaadamu.
Akihutubia kwenye chakula cha jioni kilichoandaliwa na Baraza la Mayahudi Ulimwenguni mjini Krakow, Zelensky aliwapongeza watu wa jamii nyengine ambao walijitolea maisha yao kuwaokowa Mayahudi wakati wakiandamwa na Wanazi.
"Nyinyi kwa hakika ni watu wa aina yake. Muko imara na ni mashujaa. Ni kigezo cha kile kinachopaswa kufuatwa. Holocaust inaitwa kipindi cha giza kwenye historia ya binaadamu, lakini nyinyi ni mionzi ya jua iliyopenya kwenye giza hilo," alisema Zelensky, ambaye mwenyewe ana asili ya Kiyahudi na jamaa zake ni miongoni mwa waliouawa kwenye kambi hiyo ya Auschwitz.
Uholanzi yaomba radhi
Naye Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte, alitumia hotuba yake kukumbuka siku hii kwa kuomba radhi kutokana na jukumu la nchi yake kwenye mauaji hayo ya maangamizi, na vile kutokuchukuwa hatua kuyazuwia.
"Tukiwa na manusura hawa wachache waliobakia nasi leo, naomba radhi kwa niaba ya serikali kwa vitendo vya serikali ya wakati huo. Mwaka 1995 akiwa nchini Israel, Malkia Beartix na pia Waziri Mkuu Balkenende mwaka 2005 walielezea makosa yaliyofanywa na serikali ya Uholanzi, lakini leo nataka kuwa muwazi zaidi, wakati manusura hawa wa mwisho wakiwa nasi," alisema Rutte.
Ingawa serikali kadhaa za Uholanzi zimewahi kuomba radhi kwa jinsi Mayahudi walionusurika maafa ya Vita vya Pili vya Dunia walivyotendewa waliporejea kutoka makambi ya mateso, lakini zilikuwa zikijitenga na kulaani jukumu la nchi hiyo kwenye mauaji ya Mayahudi na makundi mengine ya wachache wakati wa ukaliwaji wa jeshi la Kinazi la Ujerumani. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa nchi hiyo kutoa kauli ya kuomba radhi hadharani.
Kiasi cha Mayahudi laki moja na elfu mbili, miongoni mwa milioni sita waliouawa wakati wa Holocaust kote Ulaya, walitokea Uholanzi.
Katika kambi hiyo ya Auschwitz pekee, waliuawa watu milioni moja na laki moja, wengi wao wakiwa Mayahudi. Kambi hiyo ilikombolewa na jeshi la Kisovieti tarehe 27 Januari 1945.