1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaikaribisha 2025 kwa shangwe, hofu na matumaini

Hawa Bihoga
1 Januari 2025

Dunia imeukaribisha mwaka wa 2025, na kuuaga 2024 ulioshuhudia heshima ya Olimpiki, kurudi kwa kishindo kwa Donald Trump, na machafuko katika Mashariki ya Kati na Ukraine.

https://p.dw.com/p/4oiSw
Tokyo , Japan | Sherehe ya Mwaka mpya
Wakati Tokyo ilisherehekea kuwasili kwa 2025 kwa rangi, theluji ilitatiza safari za ndege kaskazini mwa Japani.Picha: Kim Kyung-Hoon/REUTERS

Ni wazi kabisa kwamba mwaka wa 2024 utaingia katika historia kama mwaka wa joto zaidi kuwahi kurekodiwa, huku majanga yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi yakiharibu maeneo kuanzia tambarare za Ulaya hadi Bonde la Kathmandu.

Sydney — inayojivunia kuwa "mji mkuu wa Mwaka Mpya duniani” — ilirusha tani tisa za fataki kutoka Jumba lake maarufu la Opera na Daraja la Bandari usiku wa manane saa za eneo hilo.

Maonyesho ya kuvutia ya fataki yaliangaza Bandari ya Victoria huko Hong Kong saa tatu baadaye huku Asia ikiungana kufurahia shamrashamra za Mwaka Mpya.

Maelfu walifurika mitaa ya Taipei kushuhudia jengo refu zaidi la Taiwan likiwaka kwa maonyesho ya kuvutia ya fataki.

Justin Chang, mwanafunzi wa chuo kikuu anayesomea kemia, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa anatumaini "kusoma vizuri na kupata pesa zaidi” mwaka wa 2025.

Kwenye Bandari ya Sydney yenye mandhari nzuri, wengi waliokuwa wakisherehekea walifurahia kuona miezi 12 iliyopita ikipita.

Austalia Sydney Fataki za mwakampya
Sydney ikiupokea 2025Picha: Bianca De Marchi/AAP via REUTERS

"Itakuwa vyema kama dunia ingejirekebisha yenyewe,” alisema Stuart Edwards, mfanyakazi wa bima mwenye umri wa miaka 32, kabla ya maonyesho ya fataki.

Soma pia:Kansela Scholz: 'Tunaweza kufanya 2025 kuwa mwaka mzuri'

Taylor Swift alihitimisha ziara yake ya Eras mwaka huu, kiboko mdogo aitwaye Moo Deng alivuma mitandaoni, na kipaji cha soka kijana Lamine Yamal aliisaidia Uhispania kushinda michuano ya Euro.

Olimpiki za Paris ziliunganisha ulimwengu kwa wiki chache za kipekee mwezi Julai na Agosti.

Wanariadha waliogelea kwenye Mto Seine, wakakimbia katika vivuli vya Mnara wa Eiffel, na wakapanda farasi kwenye uwanja uliopambwa wa Jumba la Versailles.

Ilikuwa mwaka wa uchaguzi wa kimataifa, ambapo mamilioni walipiga kura katika nchi zaidi ya 60.

Vladimir Putin alishinda katika uchaguzi wa Urusi uliokosolewa pakubwa kuwa wa udanganyifu, huku mapinduzi ya wanafunzi yakimwondoa waziri mkuu wa Bangladesh madarakani.

Hata hivyo, hakuna kura iliyofuatiliwa kwa karibu kama ile ya Novemba 5, ambayo hivi karibuni itamrudisha Trump Ikulu ya Marekani.

Kuanzia Mexico hadi Mashariki ya Kati, kurudi kwake kama Amiri Jeshi Mkuu tayari kunaathiri mambo.

Rais mteule ametishia kuongeza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya China na anajigamba kuwa anaweza kumaliza vita vya Ukraine ndani ya "masaa 24”.

Mabadiliko ya serikali yanakaribia pia nchini Ghana, ambako rais mteule John Mahama ataapishwa Januari 7, hali ambayo imewapa wengi matumaini ya mwaka 2025.

Silvester - Berlin
Ishara inayosema 'Karibu 2025' ilionyeshwa kwenye lango la Brandenburg kwa zaidi ya watu 65,000 walioshiriki fataki.Picha: Jörg Carstensen/dpa/picture alliance

"Mpito wa amani baada ya uchaguzi ulinipa matumaini kwamba labda mambo yataboreshwa kwa watu kama mimi,” alisema Kwesi Antwi, mwenye umri wa miaka 26, mhitimu asiye na ajira, alipokuwa akizungumza na AFP katika mji mkuu Accra, huku fataki na muziki vikishamiri.

Soma pia:Wahamiaji wengi waliangamia baharini wakienda Uhispania 2024

Machafuko yalienea Mashariki ya Kati, huku Bashar al-Assad akikimbia Syria, Israel ikiingia Kusini mwa Lebanon, na vifaa vilivyotegwa mabomu vikiripuka katika wimbi la mauaji ya Israel dhidi ya Hezbollah.

Raia walichoshwa na vita visivyokwisha huko Gaza, ambako upungufu wa chakula, makazi, na dawa uliifanya hali ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi.

"Naomba usalama na amani virejee, na vita vimalizike hatimaye,” alisema Wafaa Hajjaj kutoka Deir el-Balah, ambako maelfu ya wakazi waliokosa makazi sasa wanakaa kwenye mahema yaliyojaa.

Kulikuwa na matumaini na wasiwasi mwaka mpya ulipokaribia Syria, ambayo bado inaendelea kuyumba baada ya waasi wanaoongozwa na kundi la Kiislamu kumwondoa madarakani Assad.

"Tulihisi hofu ya kutoka mwaka huu kwa sababu ya hali ya usalama, lakini tuliamua kushinda hofu zetu,” alisema wakili Maram Ayoub, mwenye umri wa miaka 34, kutoka mji mkuu Damascus.

Syria Damascus - sherehe za kuondolewa Assad
Syria imemaliza mwaka wa 2024 kwa mshangao baada ya waasi kufanikiwa kumuondoa Bashar al-Assad kufuatia vita vya miaka 13.Picha: OMAR HAJ KADOUR/UPI Photo/IMAGO

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unakaribia kutimiza miaka mitatu mnamo Februari.

Ukraine, ikiwa na silaha chache upande wa mashariki, sasa inakabiliana na utawala wa Trump unaoonekana kuwa na nia ya kupunguza msaada wa kijeshi muhimu.

Katika hotuba yake ya Mwaka Mpya, Putin hakutaja moja kwa moja vita, lakini aliwasifu wanajeshi wa Urusi kwa "ujasiri na ushujaa” wao.

Mitaani Kyiv, mwalimu Kateryna Chemeryz alitamani "amani ipatikane hatimaye kwa Ukraine.”

Kwa maendeleo ya AI yanayokaribia na mfumuko wa bei ukitarajiwa kupungua, kuna mengi ya kutarajia mwaka 2025.

Wapenzi wa soka watagundua Kombe la Dunia la Klabu lenye timu 32, litakalofanyika Marekani katika ratiba iliyoshughulika tayari.

Zaidi ya watu milioni 400 wanatarajiwa kuhudhuria tamasha la Kumbh Mela kwenye kingo takatifu za mito ya India — tukio kubwa zaidi la wanadamu duniani.

Mamlaka ya hali ya hewa ya Uingereza tayari imebashiri joto kali duniani kwa mwaka 2025, ikipendekeza kuwa huenda ukawa mmoja wa miaka yenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa.

Sikiliza: 

2024 ulikuwa mwaka wa damu na mauti Mashariki ya Kati

Hata hivyo, utabiri wa hali mbaya ya hewa nchini Scotland ulisababisha kufutwa kwa sherehe za Hogmanay jijini Edinburgh, kivutio kikuu cha watalii ambacho kilitarajiwa kuvutia watu 50,000.

"Ni uamuzi mgumu sana unaopaswa kufanywa,” alisema mkurugenzi mwenza wa Hogmanay Al Thompson kwa AFP. "Hakuna anayependa kuwa katika hali hii.”

Kulikuwa na sherehe chache pia katika eneo la Mayotte la Bahari ya Hindi, ambapo Kimbunga Chido kiliharibu sehemu hiyo maskini zaidi ya Ufaransa katikati ya Desemba, kikiua watu wasiopungua 39.

"Tuna watoto waliopatwa na mshtuko kutokana na Kimbunga Chido, kwa hivyo hatujapanga lolote kwa usiku wa leo,” alisema Nouria Rama, mwenye umri wa miaka 45, mfanyakazi wa bodi ya elimu ya kisiwa hicho.

Kaskazini mwa Ufaransa, watu wenye ujasiri walivaa mavazi ya jadi ya kuogelea kuingia kwenye maji baridi ya Ujia wa Bahari ya Kiingereza katika uogeleaji wa kawaida mwisho wa mwaka.

Ufaransa Paris 2024 | Kanisa kuu la Notre Dame muda mfupi kabla ya kufunguliwa tena
Mwaka 2004 ulishudia kufunguliwa upya kwa Kanisaa Kuu la Notre-Dame lililoharibiwa na moto miaka mitano iliyopita.Picha: Lionel Urman/ABACAPRESS.COM/picture alliance

Wakati huohuo, kaskazini mwa Japan, theluji nzito ilikwamisha baadhi ya wasafiri kwenye viwanja vya ndege, huku safari za ndege zikifutwa.

Kwa mauzo ya magari ya umeme yanayoongezeka na nishati mbadala inayopanda, kuna matumaini kidogo kwamba maendeleo ya polepole kuhusu mabadiliko ya tabianchi huenda yakapata msukumo mwaka 2025.

Kwenye masoko ya hisa, Wall Street na masoko makuu ya Ulaya yalimaliza mwaka kwa faida nzuri, huku wawekezaji wakitazamia athari za sera za Trump kwenye uchumi wa dunia.