Dunia inasubiri kwa hamu mkutano kati ya Trump na Kim
11 Juni 2018Wakati huo huo maafisa wa nchi zote wanatafuta kupunguza tofauti zao juu ya vipi kumaliza mkwamo wa kinyuklia katika rasi ya korea.
Lakini waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo imetoa ishara ya tahadhari kabla ya mkutano huo wa kwanza kufanyika kati ya viongozi wa Marekani na Korea kaskazini kesho Jumanne, akisema kwamba inapaswa kusubiri kuona iwapo Kim ni mkweli juu ya kuwapo kwake tayari kusitisha shughuli za kinyuklia.
Mazungumzo ya dakika za mwisho kati ya pande hizo mbili yalifanyika katika taifa hilo kwa lengo la kuweka misingi ya mkutano baina ya Trump na Kim, mkutano ambao ulikuwa hakuna aliyeweza kuufikiria miezi michache iliyopita wakati viongozi hao wawili walipokuwa wakitupiana matusi na vitisho ambavyo viliongeza hofu ya vita.
Lakini baada ya wimbi la mazungumzo ya kukaribiana kidiplomasia na kupunguza hali ya wasi wasi katika miezi ya hivi karibuni, viongozi hao wawili hivi sasa wanaelekea kufanya kitendo cha kihistoria cha kushikana mikono ambapo maafisa wa Marekani wanatumai hatimaye kutasababisha katika kusitisha kabisa mpango wa kinyuklia wa Korea kaskazini ambao unaitishia Marekani.
Akitoa hali ya mkutano huo kwa waandishi habari katika mkesha wa mkutano wenyewe, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo alisema mkutano huo unaweza kutoa fursa ambazo hazikutarajiwa kubadilisha hali ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuleta amani na usitawi , kwa Korea kaskazini.
Kuondoa silaha za kinyuklia katika rasi ya Korea
Hata hivyo, hakuzungumzia kwa hamasa kubwa uwezekano wa upatikanaji wa mapatano ya haraka na kusema mkutano huo wa kilele unapaswa kuweka mwongozo kwa ajili ya "kazi ngumu inayofuata", akisisitiza kwamba Korea kaskazini inapaswa kuelekea katika kuondoa kabisa bila kurudi nyuma silaha za kinyuklia.
"Kutokana na makubaliano hafifu ambayo Marekani ilifikia katika miaka iliyopita, rais atahakikisha hakuna makubaliano yatakayofikiwa ambayo yatakosa kuzungumzia kwa kina, kitisho cha Korea kaskazini. Lengo kuu la kuwa na mahusiano ya kidiplomasia na Korea kaskazini halijabadilika.
Mpango kamili utakaoweza kufanyiwa uchunguzi wa kina wa kuondoa kabisa silaha za kinyuklia katika rasi ya Korea ni matokeo pekee ambayo Marekani itayakubali. Vikwazo dhidi ya Korea kaskazini vitaendelea hadi pale nchi hiyo itakapokamilisha kuondoa kabisa mpango wake wa silaha za kinyuklia. Iwapo diplomasia haitakwenda katika njia sahihi na tunamatumaini kwamba itaendelea vizuri, hatua hizo zitaongezeka."
Korea kaskazini hata hivyo imeonesha nia hafifu ya kuachana na silaha zake za kinyuklia ambazo inaziona kuwa muhimu kwa ajili ya uhai wa utawala wa ukoo wa Kim. Ikulu ya Marekani ya White House ilisema baadaye kuwa majadiliano na Korea kaskazini yamekwenda kwa kasi sana kuliko ilivyotarajiwa na Trump ataondoka Singapore usiku wa jumanne mara baada ya mkutano huo. Alipangiwa hapo mapema kuondoka Jumatano.Naye Kim anatarajiwa kuondoka kurudi Pyongyang Jumanne jioni.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman