DUESSELDORF:Waarabu waliotaka kushambulia maeneo ya Wayahudi Ujerumani wafungwa jela.
26 Oktoba 2005Waarabu wanne waliokuwa wanatuhumiwa kupanga kushambulia maeneo ya Wayahudi nchini Ujerumani,wamehukumiwa vifungo kati ya miaka mitano na minane jela.
Watuhumiwa watatu katika kundi hilo,wametiwa hatiani kwa kuunga mkono kikundi cha kigaidi cha al-Tawhid,ambacho kinasadikiwa kinauhisiano wa karibu na al-Qaeda.
Kikundi hicho cha Al-Tawhidi kinaongozwa na Abu Musab al-Zarqawi,anayesakwa kwa udi na uvumba kutokana na kuongoza wapiganaji wanaoendesha mashambulio nchini Iraq.
Washtakiwa hao raia wawili wa Jordan,Mpalestina mmoja na Mualgeria,walikamatwa mwezi wa Aprili mwaka 2002,baada ya polisi kuendesha operesheni kali ya kuwasaka.
Ushahidi katika kesi hiyo uliegemea zaidi maelezo yaliyotolewa na mtu mmoja aliyekamatwa siku moja na watu hao,ambaye alidai aliwahi kuwa mlinzi wa karibu wa Osama bin Laden.
Upande wa utetezi umemuita mtu huyo ni muongo kupindukia.