1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yaingia Baraza la Haki za Binaadamu la UN

17 Oktoba 2017

Marekani, Uingereza na wanaharakati duniani wamepinga kuchaguliwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuingia kwenye Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kwa rikodi mbaya dhidi ya haki hizo.

https://p.dw.com/p/2lwpt
Schweiz Genf UN Menschenrechtsrat
Picha: picture-alliance/Photoshot/X. Jinquan

"Yafuatayo ni mataifa 15 ambayo yamechaguliwa kuwa wajumbe wa Baraza la Haki za Binaadamu kwa miaka mitatu kuanzia tarehe 1 Januari 2018: Afghanistan, Angola, Australia, Chile, The Democratic Republic of the Congo, Mexico, Nepal, Nigeria, Pakistan, Peru, Qatar, Senegal, Slovakia, Uhispania na Ukraine. Nayapongeza mataifa haya ambayo yameteuliwa kuwa wajumbe wa Baraza la Haki za Binaadamu," Sacha Sergio Llorentty Soliz, balozi wa Bolivia kwenye Umoja wa Mataifa aliwaambia wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa sasa mataifa hayo 15 ndio wawakilishi wa Umoja huo kwenye chombo hicho kinachoshughulikia masuala ya haki za binaadamu. 

Kongo imepata nafasi hiyo bila kuwa na mshindani, ikipewa kura 151 za wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hatua ambayo imekosolewa vikali na Uingereza, Marekani na makundi ya kutetea haki za binaadamu. Mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa katika shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch, Louis Charbonneau, alikielezea kitendo cha kuichagua Kongo kwenye baraza hilo kuwa ni cha aibu.

Akiandika muda mchache baada ya Kongo kutangazwa, Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa, Matthew Rycroft, aliorodhesha masuala ya ukandamizaji wa kisiasa, mashambulizi dhidi ya raia, na makaburi ya pamoja, akisema kwamba kwa yote yaliyotokea mwaka jana, "kuichagua Kongo kuingia kwenye Baraza la Haki za Binaadamu lilikuwa jambo linaloudhi." 

Kuna visa zaidi ya 5,000 vilivyorikodiwa na mashirika mbalimbali ya haki za binaadamu katika kipindi cha mwaka jana pekee, ambavyo vinaonesha kiwango kikubwa cha uvunjwaji wa haki za binaadamu na mateso.

Zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na ghasia za kisiasa na wanamgambo, baada ya Rais Joseph Kabila kukataa kuondoka madarakani mwezi Disemba mwaka jana.

Marekani yalaani

Schweiz UN Menschenrechtsrat Nikki Haley
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, anataka uchaguzi wa kuingia Baraza la Haki za Binaadamu uwe wa ushindani.Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrin

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, ambaye ametoa wito wa kura za kuingia baraza hilo la haki za binaadamu kuwa za ushindani, alisema kuingizwa kwa Kongo kwenye chombo hicho kunaiathiri heshima ya baraza hilo. 

"Nchi ambayo inavunja vibaya haki za binaadamu nyumbani kwake haipaswi kuwa kwenye nafasi ya kulinda haki za binaadamu kwa wengine," alisema Haley kwenye ripoti yake. 

Marekani inaripotiwa kuhakiki upya uwanachama wake kwenye baraza hilo, baada ya hivi karibuni kujiondoa kwenye Shirika la Elimu, Utamaduni na Sayansi la Umoja wa Mataifa (UNESCO), likilalamikia mtazamo wa shirika hilo kuelekea mzozo wa Palestina na Israel. 

Tayari utawala wa Trump umetoa kauli zinazofanana na hizo kwenye dhidi ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, ukitaka mageuzi kung'oa kile unachokiita "chuki kubwa dhidi ya Israel."

Hata hivyo, si kuchaguliwa kwa Kongo pekee kuingia kwenye chombo hicho kulikokosolewa.

Mkuu wa taasisi isiyo ya kiserikali iitwayo UN Watch, Hillel Neuer, amezitaja pia Qatar na Pakistan, akisema kuwa kuziweka nchi hizo pamoja na Kongo kwenye nafasi ya uhakimu wa haki za binaadamu ni sawa na kumuweka mgonjwa aliyekufa ganzi kuwa mkuu wa kuzima moto.

Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa huundwa na wajumbe kutoka mataifa 47 wanchama wa Umoja huo ambao hupatikana kupitia kura za moja kwa moja na za siri.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Caro Robi