DR Congo: Vikosi vya EAC havijafanikiwa kuwadhibiti waasi
16 Machi 2023Christophe Mboso, Spika wa Bunge la Kongo, alionyesha picha mbaya ya kuwepo wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huko Kivu Kaskazini, mkoa ulio chini ya mashambulizi wa waasi wa M23 ambao Umoja wa Mataifa tayari umesema wanaungwa mkono na Rwanda.
Akiwahutubia wabunge pamoja na maseneta, Mboso alisisitiza kwamba kazi ya vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuungana na jeshi la Kongo ili kupigana na waasi, lakini sio kuwachunguza.
"Badala ya kujitolea kwenye vita, uwepo wao kwenye eneo letu umekuwa kazi bure na itabidi athari yake ichunguzwe ili kuangalia matokeo na hatua za kurekebisha zichukuliwe. Ndiyo maana natoa wito wa kuwa waangalifu," alisema Mboso.
Raia wa Kongo waomba hifadhi Tanzania
Hayo yamejiri huku waasi wa M23 ambao Kinshasa inawataja kuwa magaidi wakiendelea kuyadhibiti maeneo matatu kati ya sita ya mkoa wa Kivu Kaskazini. Kwa upande wake Modeste Bahati Lukwebo, Spika wa Baraza la Seneti, alichukuwa pia fursa hiyo kutoa wito kwa Wakongo kumuunga mkono Rais Felix Tshisekedi katika juhudi zake za kutafuta amani mashariki mwa nchi hii.
"Hii ni fursa kwangu kuwaalika wananchi wa Kongo kwa jumla kumuunga mkono kiongozi wa taifa ambaye anafanya juhudi zote ili usalama, utawala bora na amani kamili kutawala nchini mwetu. Na huo ndio muktadha wa ziara ya wabunge niliyoifanya hivi karibuni," aliongeza Bahati
Wabunge pamoja na maseneta wamerejea kazini miezi michache kabla ya uchaguzi unaotarajiwa hapa na ambapo shughuli ya kuwaandikisha wapigakura ikikamilika. Lakini tume ya pamoja ya uangalizi wa makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti imebainisha kasoro kadhaa ambazo zinahitaji kusahihishwa.
Uchaguzi mkuu ujao wa Kongo umepangwa kufanyika Desemba 20. Uchaguzi ni ni pamoja na wa rais, wabunge wa kitaifa na wa majimbo, pamoja na uchaguzi wa manispaa.
Mwandishi: Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.