Donald Trump kuhutubia Mkutano wa Davos
23 Januari 2025Jina la Trump limekuwa likitajwa katika, karibu kila mazungumzo katika kitongoji hicho cha Davos, mnamo wiki hii. Msomi wa chuo kikuu cha Harvard cha nchini Marekani na mtaalamu anayehudhuria kongamano la Davos mara kwa mara, Graham Allison amesema hatimaye Davos itamsikia Trump wakati atakapozungumza kwenye mkutano huo hii leo Alhamisi kwa njia ya video, huku nafasi ya kuuliza maswali ikitolewa kwa wakurugenzi wakuu wa benki na sekta ya mafuta kwa rais huyo wa Marekani ambaye, mwenyewe ni mfanyabiashara aliyetajirika kutokana na kuwekeza katika mali isiyohamishika kama majumba na viwanja.
Tayari Trump ameshatoa kionjo kwa jukwaa la Davos juu ya kile kitakachotegemewa kutoka kwake tangu alipoapishwa siku ya Jumatatu, ambayo ilikuwa pia ni siku ya kwanza ya kufunguliwa Mkutano wa Jukwaa la kimatifa la Uchumi, vionjo hivyo ni pamoja na vitisho vya kuziwekea ushuru bidhaa za Mexico na Canada, kujiondoa kwa Marekani kutoka kwenye makubaliano ya hali ya hewa ya Paris, kuuchukua Mfereji wa Panama, miongoni mwa hatua zingine anazopanga kuzichukua.
Soma Pia: Hatua za Trump zaendelea kuibua hisia mseto, Davos
Mjumbe wa Marekani Richard Grenell alimwambia katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte kwamba washirika wa jumuiya hiyo wanapaswa kuongeza michango kwa ajili ya matumizi ya ulinzi na kabla ya kufikiria kuupanua muungano huo.
Washirika wa kibiashara wa Marekani na wapinzani tayari walijibu mjini Davos mapema wiki hii, wakati ambapo wanajiandaa kwa awamu ya pili ya sera ya Donald Trump ya Marekani Kwanza.
Bila kutaja jina la Trump, Makamu wa Rais wa China Ding Xuexiang, alitahadharisha kwamba "hakuna mshindi katika vita vya kibiashara".
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisisitiza kutetea biashara huria lakini pia akaashiria hatua za maridhiano, kwa kusema kwamba alikuwa na mazungumzo mazuri ya awali na Trump.
Mkuu wa Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen amesema Umoja wa Ulaya uko tayari kuzungumza na Trump, lakini pia alisisitiza sera ya umoja huo ya kutofautiana naye kuhusu maswala ya hali ya hewa, akisema kuwa Umoja wa Ulaya utashikamana na makubaliano ya Paris.
Soma Pia: Kansela Scholz wa Ujerumani ameapa kutetea biashara huria Ulaya
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Asaad al-Shaibani amesema anataka vikwazo vya kiuchumi dhidi viondolewe, akisema kuwa huo ndio "ufunguo" wa kurejesha utulivu katika nchi iliyoharibiwa na vita.
Hata hivyo jumuiya ya kimataifa inasita kuchukua hatua za kuviondoa vikwazo hivyo, huku nchi kadhaa pamoja na Marekani zikisema zinasubiri kuona jinsi watawala wapya wa Syria wanavyotumia mamlaka yao kabla ya kufanya hivyo.
Kwa wiki kadhaa, mamlaka mpya ya Syria imekuwa ikiyashawishi madola ya Magharibi kufuta vikwazo vilivyokuwa vimeulenga utawala wa Assad kutokana na ukandamizaji wake wa kikatili wa mwaka 2011 dhidi ya maandamano ya kuipinga serikali, ambayo yalisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewataka viongozi wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara katika mkutano huo wa Jukwaa la Uchumi Duniani kuweka uangalizi wa karibu juu ya maendeleo ya akili mnemba, akionya kuwa teknolojia inaweza kuzidisha "mgogoro unaokuwa kuhusu kutofautisha kati ya taarifa za kweli na taarifa potofu".
Vyanzo: AFP/RTRE