IS yaudhibiti mji wa Mheen nchini Syria
2 Novemba 2015Kwa mujibu wa waangalizi wa haki za binadamu nchini humo, wanamgambo hao walifanikiwa kuudhibiti mji wa Mheen,ulioko kilomita 24 magharibi mwa Damascus.
Kabla ya kundi hilo la dola la kiisilamu kufanikiwa kuudhibiti mji huo lilipata upinzani mkali toka kwa vikosi vya serikali nchini humo. Eneo hilo ni eneo muhimu kwa upande wa serikali ya Syria.
Kundi hilo la dola la kiisilamu limezidi kujiiimarisha nchini humo katika kipindi cha mwaka huu baada ya kufanikiwa kuyadhibiti maeneo muhimu nchini humo ikiwa ni pamoja na eneo la Palymira.
Aidha mgogoro kati ya waasi na serikali ya nchi hiyo unaonekana kutofikia kikomo licha ya mikakati inayozidi kuwekwa ya kumaliza mgogoro huo kufuatia mazungumzo yaliyomalizika mjini Vienna ijumaa iliyopita yaliyoihusisha pia Iran kwa mara ya kwanza.
Iran yataka kuitishwa kwa uchaguzi nchini Syria
Iran hadi sasa inasisitiza kufanyika kwa uchaguzi nchini humo kama njia moja wapo ya kutatua mgogoro huo hatua ambayo inaonekana kupingwa vikali na makundi ya upinzani nchini humo yakisema hizo ni mbinu zinazotumika za kutaka kumbakisha madarakani Rais Bashar al- Assad.
Mkutano wa Vienna ulimalizika kwa kutoa mwito wa kukomesha mapigano nchini humo lakini kikwazo kikubwa kinabaki kuwa miongoni mwa makundi yanayounga mkono pande zinazopingana nchini humo.
Mgogoro huo umezidi kuendelea kufukuta hasa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita baada ya Urusi kuanzisha mashambulizi ya anga nchini humo kwa lengo la kumuunga mkono Rais Assad.
Wakati mataifa ya Marekani na Urusi yanaonekana kuziunga mkono pande mbili tofauti zinazopingana nchini humo ambazo ni kundi la waasi lililojiimarisha upande wa magharibi na serikali ya nchi hiyo lakini bado mataifa hayo kila moja kwa upande wake yanapambana dhidi ya kundi la dola la kiisilamu ambalo limedhibiti eneo kubwa la upande wa mashariki na kaskazini nchini humo.
Kundi hilo la dola la kiisilamu ambalo linapambana dhidi ya pande zote mbili za waasi na magharibi mwa Syria na majeshi ya serikali tayari vimeanzisha mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya nchi hiyo tangu serikali ya nchi hiyo ilipoanzisha mashambulizi dhidi yake mashariki mwa mji wa Allepo kwa msaada wa ndege za kivita za Urusi.
Mgogoro huo wa Syria ambao umedumu kwa muda wa miaka minne hadi sasa umesababisha vifo vya watu 250,000.
Mwandishi: Isaac Gamba/DPAE/RTRE
Mhariri :Yusuf Saumu